Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana( CMSA) imezindua wa Hatifungani ya Benki ya NMB ya miaka 10 yenye jumla ya thamani ya Sh.trilioni moja na mauzo ya toleo la kwanza la hatifungani hiyo yenye mguso na matokeo chanya kwa jamii.

Akizungumza leo Septemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama amesema mamlaka hiyo ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini.

Ameongeza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Hatifungani zinazouzwa kwa umma zinakidhi matakwa ya sheria, taratibu na kanuni za uuzaji wa hatifungani kwa umma na kukidhi viwango vya kimataifa.

"Agosti 31 2023, CMSA iliidhinisha Waraka wa Matarajio wa Benki ya NMB kuuza Hatifungani ya miaka 10 yenye jumla ya thamani ya shilingi trilioni moja (Tsh 1,000,000,000,000).

" Kwa mujibu wa taratibu za masoko ya mitaji, CMSA inatoa taarifa rasmi kwa umma kuwa Benki ya NMB imepata idhini ya CMSA kutoa hatifungani itakayotolewa katika fedha za aina mbalimbali na hatifungani hii itakuwa na mguso na matokeo chanya katika maeneo mbalimbali.

"Hatifungani hii inaweka historia ya kuwa hatifungani kubwa zaidi (bigger ticket size) kutolewa nchini Tanzania na katika Ukanda Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa kuzingatia kuwa, Hatifungani hii inatolewa katika fedha za aina mbalimbali, tunatarajia kuwa itachangia katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni hapa nchini, " amesema.

Amefefanua idhini hiyo imetolewa na CMSA baada ya Benki ya NMB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani.

Pia uwepo wa Muundo wa Hatifungani yaani Bond Framework ulioandaliwa na benki ya NMB kwa kushirikiana na Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Barani Afrika (FSD Africa) na kukidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji.

Na hatimaye kupata ithibati kutoka kwa kampuni ya Sustainalytics ya nchini Uingereza, yenye utaalam kuhusu miradi endelevu kwa maendeleo ya jamii.

CPA Mkama amesema mchakato wa kuidhinisha hatifungani unahusisha taasisi na wataalam mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mshauri kiongozi wa benki ya NMB, Absa Bank Tanzania Limited; Kampuni ya Ushauri katika Masoko ya Mitaji, Orbit Securities Company Limited; Mshauri wa Sheria, Rex Attorneys.

Pia Mkaguzi na Mtoa Taarifa za Hesabu, KPMG; Taasisi ya Ushauri kuhusu muundo wa Hatifungani, FSD Africa; na Taasisi ya utoaji wa ithibati katika kukidhi matakwa ya miongozo ya jumuiya ya kimataifa katika masoko ya mitaji, Sustainalytics.

Akieleza zaidi amesema mauzo ya toleo la kwanza la Hatifungani hiyp iitwayo Jamii Bond kwenye soko la awali yanafunguliwa leo hii Septemba 25, 2023 na yanatarajiwa kufungwa Oktoba 27, 2023, ambapo benki ya NMB inatarajia kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni 75 (na uwezo wa kuchukua ziada ya shilingi Bilioni 25).

Amesema fedha zitakazopatikana kupitia hatifungani hii zitatumika kuwekeza katika miradi endelevu kwa maendeleo ya jamii yaani sustainability social projects. Baada ya muda wa mauzo kwenye soko la awali kukamilika, hatifungani hii itaorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.

"Utoaji wa hatifungani hii ni hatua muhimu katika ustawi na maendeleo ya Sekta ya Fedha na uchumi hapa nchini kwani utachangia katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

Pia hatifungani hiyo inawezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaani National Economic Empowerement Policy, kwani fedha zitakazo patikana zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii, na wananchi watakao wekeza katika hatifungani hii watalipwa riba, hivyo kuinua vipato vyao.

"Maendeleo na mafanikio katika masoko ya mitaji yanatokana na mazingira wezeshi na shirikishi ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza sera ya uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa.

" Hivyo kuwa chachu yenye matokeo chanya katika maendeleo na ustawi wa sekta ya fedha, husan masoko ya mitaji.Kutokana na chachu hiyo, sasa tunashuhudia utolewaji wa bidhaa mpya na bunifu," amesema.

Aneongeza NMB ni miongoni mwa kampuni ambazo zimetumia fursa katika masoko ya mitaji, ambapo mwaka 2008, CMSA ilitoa idhini kwa Benki ya NMB kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa DSE.

Amesema katika mauzo hayo, NMB ilifanikiwa kupata Sh.bilioni 224.9 sawa na asilimia 357 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 63. Bei ya hisa za benki ya NMB imeongezeka kwa asilimia 637 kutoka shilingi 600 kwa hisa wakati wa mauzo ya hisa ya awali, hadi shilingi 4,420 kwa hisa, leo tarehe 25 Septemba 2023.

Aidha, mwaka 2016, CMSA ilitoa idhini kwa Benki ya NMB kuuza hatifungani yenye thamani ya Shilingi Bilioni 200. Hatifungani hii iliuzwa katika matoleo manne yenye thamani shilingi bilioni 95 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 224.8 zilipatikana sawa na mafanikio ya asilimia 236.7.

"Kutokana na mafanikio hayo, Benki ya NMB imeweza kutekeleza mikakati mbalimbali iliyoleta mageuzi na mafanikio yenye tija katika utendaji wa benki na kwa wanahisa wake. Haya ni mafanikio makubwa.

"Kabla ya kuuza hisa na kuorodheshwa DSE, NMB ilikuwa ikipata hasara na hivyo kutoweza kutoa gawio kwa mwanahisa wake yaani Serikali, " amesema CPA Mkama.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Msajili Wa Hazina - Bw. Nehemiah Mchechu, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede; Afisa Mtendaji Mkuu wetu - Bi. Ruth Zaipuna; Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) – CPA. Nicodemus Mkama; Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar Es Salaam (DSE) - Bi. Mary Mniwasa; pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kushoto), akipokea Waraka wa Matarajio ya Programu ya Utoaji wa Hati Fungani ya Muda wa Kati (MTN) kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, wakati wa uzinduzi wa NMB Jamii Bond.








Wageni waalikwa kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.



Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama akizungumza jambo mbele ya wagani waalikwa mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Hatifungani ya Benki ya NMB ya miaka 10 yenye jumla ya thamani ya Sh.trilioni moja na mauzo ya toleo la kwanza la hatifungani hiyo yenye mguso na matokeo chanya kwa jamii.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...