Na Mwandishi wetu, Mirerani

KAMPUNI ya Franone Mining and Gems LTD inayochimba madini ya Tanzanite kitalu D na kumiliki kitalu C imekomesha kero ya muda mrefu ya ubovu wa barabara ya kupanda na kushuka kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, baada ya ombi la Naibu Waziri Mkuu Dkt Dotto Biteko la kutengeneza barabara hiyo kutekelezwa.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita sita inajengwa na kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, baada ya Naibu Waziri Mkuu Biteko kutoa ombi hilo hivi karibuni wakati akiwa Waziri wa Madini.

Msemaji wa kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, Vitus Ndakize akizungumza na waandishi wa habari amethibitisha kutengenezwa kwa barabara hiyo.

Ndakize amesema baada ya kusikiliza ombi la Waziri Biteko walikaa kama kampuni na kuridhia kutengenezwa kwa barabara hiyo inayotumiwa na wachimbaji madini wengi wa Tanzanite.

Amesema waliwashirikisha wakala wa barabara za mjini na vijijini (Tarura) wilaya ya Simanjiro, kwa lengo la kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango sahihi cha changarawe.

"Kwetu hii ni sawa na kutoa huduma kwa jamii inayotuzunguka (CSR) kwani wachimbaji wengi watatumia barabara hii kwa kutumia magari na pikipiki zao," amesema Ndakize.

Hivi karibuni mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining and Gems LTD Onesmo Mbise, ameeleza kuwa wametenga kiasi cha Sh171 milioni kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo.

Dereva wa kuendesha pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) ndani ya ukuta unaozunguka migodi hiyo, Jaqcline Chacha ameishukuru kampuni ya Franone kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo.

"Awali barabara hii ilikuwa mbovu ila baada ya Franone kutengeneza imekuwa nafuu kwetu kwani hata ukichukua pikipiki kwa mkopo na kurejesha kwa mkataba unaweza, kutokana na barabara kutengenezwa," amesema Chacha.

Mmoja kati ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite, Baraka Kayeleki amesema matengenezo ya barabara hiyo ni faida kubwa kwao kwani ubovu wake ulikuwa ni changamoto.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...