Na Mwandishi Wetu

KATIKA kuendelea kudumisha dhamira ya ubunifu wa kiteknolojia, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML)  imetoa kiasi cha Sh. milioni 150 kudhamini Maonyesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofayika mkoani Geita.

Maonyesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka, yanatarajiwa kuzinduliwa Septemba 23 na kuhitimishwa  Septemba 30 mwaka huu.

Maonyesho hayo yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), katika viwanja vya Bombambili vilivyopo eneo la Mamlaka ya Maeneo ya Usindikaji Nje (EPZA) mkoani humo.

Akizungumzia ushiriki wa GGML katika maonesho hayo mjini Geita jana, Meneja Mwandamizi wa kampuni hiyo anayesimamia mahusiano jamii, Gilbert Mworia alisema maonesho hayo yamekuwa na mvuto wa kipekee tangu yalipoasisiwa kutokana na ufadhili wa GGML kupitia mfuko wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) ambao uliwezesha ujenzi wa eneo hilo la EPZA pamoja na eneo la uwanja huo wa maonesho.

"Mbali na maonyesho, tuliwekeza Sh 800 milioni katika ujenzi wa jengo la utawala la EPZA. Tunafurahi kuona mpango wetu wa EPZA mkoani Geita unastawi na kutimiza malengo ya jamii ya wana-Geita kikamilifu," alisema na kuongeza;

"Msaada wetu unavuka usaidizi wa kifedha ambao tumeendelea kuutoa kila mwaka, kwa sababu tulitoa msaada wa maandalizi ya maonesho hayo kama vile mahema, jenereta la dharura na mafuta yanakayotumika kwa wakati wote wa maonesho,” alisema Mworia.

Alisema katika kipindi cha miaka sita ya ushirikiano huo na wadau wa maonesho hayo, GGML imeendelea kuelimisha jamii kuhusu teknolojia inayotumika katika vifaa vya uchimbaji madini hali inayoendelea kukuza uhusiano imara kati yake, kampuni za ndani na wachimbaji madini.

Aidha, alisema ili kutimiza malengo ya muda mrefu ya ukuaji wa uchumi endelevu, GGML inaunga mkono Dira ya 2025 ya serikali. Mpango huu unalenga kuiwezesha sekta ya uchimbaji madini kukua na kufikia kiwango cha asilimia 10 kwenye Pato la Taifa la Tanzania.

Ufunguzi rasmi wa Maonesho hayo ya 6 ya Madini na Teknolojia mkoani Geita utafanywa na Dk. Dotto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Septemba 23 na yatafungwa Septemba 30 mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan. Kauli mbiu ya maonesho hayo inasema  Matumizi ya teknolojia sahihi katika kuinua wachimbaji wadogo kiuchumi na kuhifadhi mazingira.


Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong (kulia) akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa kitengo cha huduma za dharura cha kampuni hiyo pindi waliposhiriki maonesho hayo mwaka jana. Kushoto ni Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...