*Dkt.Mollel abainisha mafanikio ya Wizara na maboresho sekta ya afya

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV

 SERIKALI imesema bado kuna idadi ndogo ya wananchi waliojiunga kupata bima ya afya hali  inayosababisha kuwepo kwa changamoto katika utoaji wa huduma za matibabu na baadhi yao kukataka bima wakiwa tayari wanaugonjw.

Pia ilisema hadi sasa kuna  idadi ndogo ya watoto waliochini ya miaka 18 waliopata toto afya kadi .

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam  katika kuelezea mafanikio yaliyopatikana sekta ya afya  kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali, Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel alisema hivi sasa idadi inaonyesha  kuna jumla ya watoto milioni 31 walio chini ya miaka 18.

Alisema kati ya hao watoto waliopata kadi za toto afya ni 210,000 tu na waliobaki hawapo katika mfumo huo.

Dk. Mollel alisema watoto hao wenye kadi toto walichangia milioni tano huku ghalama yao ya matibabu waliyoitumia ilikuwa ni sh. milioni 40.

Hata hivyo Dk. Mollel alisema bado kuna uitikiaji mdogo wa uandikishaji wa bima ya afya mashuleni tofauti na mategemeo waliojiwekea.

“Ili kufikia dhamira ya Serikali ya afya bora kwa wote lazima kama nchi kuwa na mfumo endelevu na imara wa uchangiaji wa gharama za matibabu (bima ya afya”kabla ya kuugua”,alisema Dk. Mollel.

Dk. Mollel alisema  Mafaniko ya Wizara Chini ya Rais Dk. Samia ameendelea kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wote kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya karibu na maeneo yao kutokana na uwekezaji uliofanywa wa ujenzi wa miundombinu ya utoaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema Rais Dk.Samia tayari amewekeza sh. trilioni 6.7 ambazo zimegusa sehemu mbalimbali katika afya ikiwemo dawa, miundombinu ya teknolojia na teknolojia tiba ambapo  awali watanzania wengi walikuwa wanatibiwa nje ya nchi .

“Kuwepo kwa vifaa bora na vya kisasa  tumepunguza ghalama ya kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi na wengi wanatibiwa nchini,”alisema

Aidha alisema kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2022 hadi Machi mwaka huu ,vituo vya kutolea huduma za afya nchini vimeongezeka kufikia 11,040 ikilinganishwa na vituo 8549 mwaka 2021.

“Juhudi hizo sasa zimewezesha sehemu kubwa ya wananchi kupata huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi ,”alisema.

Pia alisema Serikali imeendelea kukamilisha ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa mipya ambayo ni Njombe,Songwe,Geita,Simiyu,na Katavi na tayari hospitali zote zinatoa huduma.

“Licha ya kukamilika kwa hospitali zilizojengwa katika miji mipya pia serikali ya awamu ya sita inaendelea kukamilisha ujenzi wa hospitali ya rufaa Kanda ya Kusini Mtwara na hospitali ya Kanda Chato ambapo tayari huduma zimeshaanza kutolewa”alisema

Alisema hadi Machi mwaka huu Vyumba vyenye Uangalizi Maalumu (ICU) vimejengwa 73 na tayari vimeshakamilika.

Akizungumzia maboresho yaliyofanywa katika huduma za magonjwa maalum ,alisema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika eneo hilo.

Alisema hospitali za mkoa zote zimepatiwa T-SCAN na Serikali inategemea kupokea magari ya kubebea wagonjwa 720.

“Hakuna Wilaya itakayokosa usafiri wa wagonjwa kwa sababu magari yanayokuja ni mengi,”alisema.

Vilevile, katika mkutano huo, Dk. Mollel alisema Serikali imendelea kuimarisha huduma za kibingwa hapa nchini kwa kuweka utaratibu mzuri wa kusomesha watumishi ujulikanao kwa jina la Samia Health Super Specialialisation Program ambapo mwaka 2023/2024 serikali imeongeza fedha za udhamini wa masomo kufikia bilioni 9kutoka bilioni 5 iliyokuwa imetengwa mwaka 2022/2023.

Dk. Mollel alisema kutokana na kuongezeka kwa idadi na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa gharama za kumhudumia mgonjwa wa saratani ni sh.milioni 70 kwa mwaka na kusafisha damu kwa mgonjwa wa figo ni sh. milioni 36 na mgonjwa mwenye kuhitaji upasuaji wa moyo sh. milioni 13 kwa mwaka.

“Nawaomba wananchi tujenge tabia ya kuanza kubadili mitindo hatarishi ya kiafya katika maisha kwa lengo la kuepuka magonjwa magonjwa haya ambayo ;kama tutazingatia ushauri wa wataalam waafya kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi , kuepuka kunywa pombe kupita kiasi hakika tunaweza kupunguza changamoto ya magonjwa”,alisema

 

 Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na mafanikio ya Wizara hiyo jijini Dar es Salaam.


Baadhi Watendaji wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya ikiwa NHIF wakati Naibu Waziri Afya Dkt.Godwin Mollel akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...