KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetoa wito kwa Serikali kuendelea kuweka kipaumbele katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe nchini, ili kuwa Taifa lenye watu wenye afya na lishe bora na kuweza kufikia malengo endelevu.

Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo (MB) mara baada ya kufanya ziara katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa lengo la kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo.

Nyongo amesema, afua za lishe zinahitaji kuwa na uwekezaji wa kutosha na kupewa kipaumbele, kwa kuwa Taifa lisipowekeza kwenye lishe linaweza kujikuta linatibu wananchi wengi kwa sababu ya lishe mbovu na kushauri matumizi ya lishe kama Tiba namba moja yenye gharama nafuu.

“Waheshimiwa wabunge wenzangu hili halina mjadala twendeni tukaishauri Serikali tuhakikishe wanaweka kipaumbele kwenye afua za lishe, tutaendelea kutibu wananchi wengi kwa sababu ya lishe mbovu wakati lishe ni tiba namba moja tena ya bei nafuu.”Amesema Nyongo.

Pia amesisitiza elimu ya lishe kuendelea kutolewa zaidi kwa jamii ya watanzania, ikihusisha makundi yote muhimu, kwani bado kuna upotoshaji mkubwa unaofanyika kwenye masuala ya lishe.

"Elimu zaidi inahitajika kwa watanzania katika masuala ya lishe na chakula kwa ujumla wapo baadhi ya watu wanaibuka na bidhaa mbalimbali za lishe, ambazo zimekuwa na matokeo hasi kwa watumiaji na nyingine kuwaletea shida kiafya watumiaji hao." Ameeleza.

“lazima tutoe ushauri ni chakula gani watu waweze kutumia, maana sasa hivi lishe imevamiwa kila moja ameibuka na lake, sasa kila mtu ni mtaalamu wa lishe.” Ameongeza Mhe. Nyongo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema wataendelea kuimarisha eneo la lishe kutokana na kuwa ni eneo msingi kwa Taifa, pamoja na kusimamia maeneo yenye shida kwa upande wa utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe ambayo tayari yamebainishwa na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe ambayo itachukua hatua za kuboresha zaidi.

Dkt. Mollel ameiomba kamati ya Bunge kuangalia namna ya kuweza kuipatia nguvu Taasisi hivyo, kwani bado haina misuli ya kuweza kudhibiti baadhi ya masuala yanavyoibuka kila kukicha kuhusiana na masuala ya Chakula na Lishe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna akieleza utekelezaji wa Taasisi hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ameeleza kuwa elimu zaidi inaendelea kutolewa kwa watanzania.

"Tabia ya kula ni sehemu ngumu na changamoto kubwa katika suala la lishe watu wengi wanalima kwa ajili ya kuuza na sio kwa ajili ya matumizi ya familia na Kaya....Udumavu hutokea katika kipindi ambacho mtoto ni mdogo na akina Mama wengi hasa vijijini wanaingia katika shughuli za kiuchumi mapema na malezi ya watoto hudumaa wengi hulelewa na watoto au viporo." Amesema.

Dkt. Germana amesema, katika Utafiti ulioelekezwa kufanyika na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambao bado haujakamilika ulioangazia mikoa inayozalisha chakula kwa wingi, mikoa iliyopunguza uzalishaji kwa kiwango kikubwa na suala la udumavu sababu kubwa waliyogundua inayopelekea udumavu ni pamoja na malezi kwa wazazi kutokuwa na muda wa kuhakikisha watoto wanapata lishe bora pamoja na maambukizi ya maradhi ya kuambukiza ikiwemo UKIMWI katika mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya ambayo maradhi hayo husababisha changamoto katika Lishe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bw. Obbey Assery, ameiomba kamati ya kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuwa sehemu ya kuisemea lishe katika ngazi ya chini kupitia Halmashauri hadi ngazi ya Taifa (Bungeni,) na kuiomba kupigia kelele suala la kutenga shilingi 1000 za afua za lishe kwa ajili ya watoto chini ya umri wa miaka 5 ili zitumike katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe.

Kuhusiana na mabadiliko ya Sera kama ilivyoelekezwa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema; kwa kushirikiana na Wizara husika wanaangalia mabadiliko hayo ili Sera ziende sambamba na hali ya sasa na hiyo ni pamoja na kutengeneza na kuthibitisha chakula lishe na kutoa mafunzo kwa wadau na ithibati ya kutengeneza Chakula Lishe kwa ajili ya kupeleka sokoni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) akizungumza wakati wa ziara iliyofanywa na kamati hiyo katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania na kueleza kuwa afua za lishe zinahitaji uwekezaji wa kutosha na kupewa kipaumbele. Leo jijini Dar es Salaam Tanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bw. Obbey Assery akizungumza wakati ziara hiyo na kutoa rai kwa wabunge kulisemea suala la lishe katika ngazi ya Taifa (Bungeni,) na katika ngazi ya Halmashauri kupitia mabaraza ya madiwani. Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna akitoa mada kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI iliyotembelea Taasisi hiyo kwa lengo la kujifunza na kuona shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakipata maelezo kutoka wataalam wa maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ikiwa ni ziara ya kujifunza na kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Leo jijini Dar es Salaam.Matukio mbalimbali wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania. Leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...