Na Muhidin Amri,
Mbinga


MKAKATI wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kumtua mama ndoo kichwani umetekelezwa kwa vitendo kwa wakazi wa kijiji cha Kitanda Halmashauri ya mji Mbinga mkoani Ruvuma.


Hatua hiyo imetokana na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilayani Mbinga,kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaohudumia  zaidi ya wakazi 3,600 wa kijiji hicho na kijiji cha Mangwangala.


Wakizungumza jana wananchi wa kijiji hicho wamesema,kukamilika kwa mradi huo kumewaondolea changamoto ya kutafuta  huduma ya maji umbali mrefu kiasi cha kukwamisha shughuli nyingine za maendeleo na kuongeza kuwa,hiyo ni mara ya kwanza kushuhudia maji ya bomba yakitoka kwenye kijiji hicho.


Daud Mapunda alisema,baada ya kukamilika kwa mradi huo maisha yao  yatakuwa mazuri na kuimarika kwa ndoa nyingi ambazo ziliyumba kutokana na kero ya maji ambapo akina mama walitumia muda mwingi kwenda kutafuta huduma hiyo badala ya kuhudumia ndoa zao.

Athanas Mbunda mkazi wa kijiji cha Kitanda alisema,katika maisha yao yote wamekuwa na changamoto ya maji safi na salama kwa muda muda mrefu na kuna wakati walilazimika kutafuta maji mbali na kijiji chao.


Alisema,katika kutafuta huduma ya maji kuna wakati mwingine walilazimika kulala mtoni na kurudi siku ya pili yake na hivyo kusababisha migogoro kwa baadhi ya familia.


“mimi nina umri wa zaidi ya miaka 45,na katika umri wangu huu sijawahi kuona maji ya bomba hapa kijijini kwetu,tunaishukuru serikali yetu kwa kutambua changamoto  tuliyonayo na leo tumeona mradi wa maji uliotekelezwa na ndugu zetu wa Ruwasa”alisema.


Diwani wa kata ya Kitanda Aureus Ngonyani,ameishukuru Ruwasa kukamilisha mradi na serikali kutoa fedha ambazo zimemaliza kero ya huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa kijiji cha Kitanda na Magwangala.


Aidha,ameiomba serikali kupitia Ruwasa kufikisha huduma ya maji kwenye vijiji vitatu vilivyobaki ambavyo bado wananchi wake wanaendelea kuteseka kwa kukosa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.


Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala alisema,mradi ulianza utekelezwa mwezi Julai 2022 kwa kutumia mkandarasi M/S JB Mwalongo kwa gharama ya Sh.milioni 473,101,856.40.


Hata hivyo alisema, muda wa utekelezaji wake ulisogezwa mbele kwa miezi minne  zaidi kutokana na changamoto ya mvua na taratibu za msamaha wa kodi kuchelewa.


Alisema,mradi huo umekamilika tangu mwezi Juni 2023 kwa asilimia 100 na sasa uko kwenye muda wa matazamio ya mwaka mmoja na mkandarasi amelipwa Sh.milioni 257,555,604.00 ambazo ni sawa na asilimia 54.4 na  unatoa huduma kwa wananchi.


Ametaja kazi zilizofanyika ni kujenga tenki moja la lita 150,000,kuchimba mitaro na kulaza mabomba umbali wa kilomita 19,935  ujenzi wa vituo 14 vya kuchotea maji na ujenzi wa chanzo(Banio).

Sinkala alitaja madhumuni ya  kutekeleza mradi huo ni kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma ya maji iliyokuwepo,kupunguza magonjwa ya mlipuko na utasaidia watu kupata muda mwingi  wa kushugulika na kazi za zingine za kiuchumi kwani huduma ya maji itapatikana karibu na makazi yao


Tenki la kuhifadhi lita 150,000 lililojengwa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira(Ruwassa) kwa ajili ya kuhudumia zaidi ya wakazi 3,600 wa kijiji cha Kitanda na Mangwangala Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma likiwa limekamilika na kuanza kutoa huduma ya  maji safi na salama.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...