NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
UKOSEFU wa maji katika Jiji la Mwanza unaelekea kubaki historia kufuatia mitambo ya kuzalisha na kusukuma maji ya Mradi wa Maji na Kituo cha Tiba ya Maji Butimba,kufanyiwa majaribio.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amewasha moja kati ya pampu tano za mitambo hiyo,leo na kushuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),Christopher Mwita Gachuma,akiwemo Mwenyekiti wa CCM mkoani humu Ruben Sixbert,Wabunge na Wakuu wa Wilaya za Nyamagana na Ilemela.
Makalla baada ya kuwasha mitambo ya mradi huo uliofikia asilimia 96,amesema maji kwa Jiji la Mwanza ni agenda na kilio cha muda mrefu,hivyo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amekisikia na kukitatua kwa vitendo.
Amesema kukamilika kwa mradi huo ni pigo na habari mbaya kwa wapinzani wa serikali waliotarajia mradi kutokamilika na kwenda kuutumia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kama fimbo ya kuitandika CCM.
Makalla amesema mradi wa Butimba kutoa maji ni heshima kwa CCM na hata wananchi wakiulizwa wanataka nini kati ya maji na Katiba mpya watasema maji,hivyo jukumu lililobaki kwa viongozi wakawaelimishe wananchi,wawaeleze yaliyofanywa na serikali pia mabomba yaliyopokelewa yasifikishwe kimya kimya.
“Nimewasha pampu kujaribu mitambo maji yametoka,ahadi waliyoniahidi wakandarasi SOGEA SATOM imetimia na niwashukuru.Julai 31,mwaka huu, nilikuja hapa nikakasirika si Makalla aliyezoeleka, nilifanya hayo si kwa malsahi yangu binafsi bali ya Mh.Rais,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoogongwa na Rais Dk.Samia,imejiekeleza kutatua matatizo ya watu,kwa anayofanya Rais na kufahamu changamoto ya upungufu wa lita milioni 27 za maji,ametoa fedha kuboresha chanzo cha Capripoint kizalishe lita milioni 144 kukidhi mahitaji.
Ameagiza usambazaji wa maji na ujenzi wa matenki uende kasi,wabunge na madiwani wakawaambie wananchi kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita kuondoa tatizo la maji Mwanza.
Makalla amewataka wananchi kuchukua tahadhari wasinywe maji bila kuyachemsha mradi bado uko katika majaribio kwani wako watu wenye fitina watasema ni machafu.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA,Neli Msuya amesema Mradi wa Maji na Kituo cha Tiba cha Maji Butimba unaojengwa kwa sh. bilioni 70, ni mbadala wa chanzo cha Caprpoint ambacho uzalishaji wake haukidhi mahitaji ya lita milioni 165 za maji kwa Jiji la Mwanza.
“Chanzo cha Capripoint hakikidhi na kinazalisha lita milioni 90 kwa siku na kusababisha upungufu wa lita milioni 75, mgawo wa maji maeneo ya miinuko na pembezoni,hivyo awamu ya kwanza mradi wa Butimba utazalisha lita milioni 48 za maji kadhalika awamu ya pili zitazalishwa lita milioni 48 na kufikisha lita milioni 96 kwa siku,”amesema.
Msuya amesema licha ya maji kuongezeka na kufikia lita milioni 138 kwa siku bado mahitaji yapo,ili kwenda sambamba na mahitaji ya maji kwa wananchi kwa siku,chanzo cha Capripoint kitaboreshwa kizalishe lita milioni 144 kutoka lita milioni 90 za sasa.
“Mradi huu utahudumia wananchi 450,000 wa Jiji la Mwanza,tunamshukuru Mh.Rais Dk.Samia kwa kutoa fedha za mradi na mingine ili kuboresha huduma na kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi pia,tutaweka mtandao mpya wa maji na kuboresha wa zamani kupunguza upotevu wa maji na athari baada ya maji kuongezeka,”amesema.
Kwa mujibu wa Msuya makangavuke mawili (jenereta) ya kufua umeme wa dharurakatika chanzo cha Butimba unapokatika umeme wa gridi, yamesimikwa lakini yanatumia lita 10,369 za mafuta ya dizeli sawa na sh. milioni 35.4 gharama ambazo ni kubwa kwa siku.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa MWAUWASA amesema chanzo kipya cha Kabanganja kitakachozalisha lita milioni 200 kwa siku kitajengwa kwa awamu mbili,fedha zimetengwa tayari na mingine ni miradi ya haraka ya uboreshaji mifumo ya maji itakayogharimu sh. bilioni 4.3, ikikamilika yote itakidhi mahitaji ya wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya MWAUWASA,Christopher Gachuma amesema serikali imetumia fedha nyingi kujenga mradi huo na majaribio hayo ni ishara unaelekea kukamilika,hivyo wananchi waitunze miundombinu hiyo na zikipatikana bilioni 60 za vyanzo vingine zitamaliza tatizo la maji Mwanza.
Mbunge wa Nyamagana na Ilemela,Stansalu Mabula amesema CCM ililetwa kutatua changamoto za wananchi wakati wa kampeni za 2015 na 2020 kilio cha Nyamagana kilikuwa maji na kumshukuru Rais Dk.Samia kipekee na moyo wake wa dhati wa kuwezesha wananchi kupat maji.
“Ilemela kilikuwa maji na haikuwa rahisi kuwaeleza wananchi waishio kando ya Ziwa Victoria kukosa maji wakati yanafika hadi Tabora,nafarijika kushuhudia majaribio ya mitambo ikizingatiwa serikali ya awamu ya sita ilitoa ahadi nyingi na iko makini kuzitekeleza,” ameeleza Dkt. Angeline Mabula Mbunge wa Ilemela.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...