Na Mwandishi Wetu-Arusha

Mkutano wa wataalamu wa Sekta ya Mawasiliano Duniani unaoratibiwa na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kwa ushirikiano na Tanzania ujulikanao kama ITU -T SG20 unaendelea kufanyika jijini Arusha kwa wiki ya pili, ukijadili viwango vya kiteknolojia katika teknolojia za Mtandao wa Mambo(IoT), Miji na Jamii Maridadi (Smart Cities & Communities-SC&C).

ITU -T SG20 ni kikundi-kazi cha Shirika la Kimataifa la Mawasiliano kilichojikita katika sekta ya mawasiliano-pepe (ITU-T). Dhima ya kikundi kazi hicho ni kusimamia, kuandaa viwango na mapendekezo ya ubora wa mawasiliano pepe yanayotumika duniani. Aidha, ITU -T SG20 kina jukumu la kutambua na kuorodhesha mahitaji ya viwango vya Mtandao wa Mambo yaani Internet of Things (IoT), kuendeleza na kuidhinisha viwango vya IoT na miji na jamii maridadi na kushirikiana na vikundi vingine vya ITU na mashirika mengine ya viwango ili kuhakikisha kwamba viwango vya IoT na SC&C vinakidhi ubora unaokubalika kimataifa.   

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari alisema kufanyika kwa mkutano huo nchini ni suala muhimu kwa kuwa limewezesha wataalamu wengi zaidi kuhudhuria, suala litakalokuwa na manufaa kwa nchi "hii ni heshima kwa nchi yetu kupata fursa ya kuandaa mikutano hii ya kitaalamu kwa kuwa kwa kawaida hufanyika nchini Uswisi, watalaamu wetu wengi zaidi wameweza kuhudhuria suala ambalo ni afya kwa sekta ya mawasiliano nchini kwetu" alibainisha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Kisekta wa TCRA Mhandisi Mwesigwa Felician alisema ITU -T SG20 inaangazia maeneo ya IoT, miji na jamii maridadi ili kuhakikisha dunia inaweka matumizi ya teknolojia za Kidijitali zenye viwango vinavyotakiwa kwa kuzingatia ukuaji wa kasi wa teknolojia ambao dunia inaushuhudia.

“Mkutano huu unaangazia maswali saba ambayo wataalamu hapa hutoka na majibu kamili yatakayotumika kama mstari wa viwango kwa dunia nzima kwenye teknolojia ya Mtandao wa Mambo yaani IoT, maswali hayo ni pamoja na Ulinzi, faragha, uthabiti, na utambuzi wa Mtandao wa Mambo, Miji na Jamii za kidijitali; Urahisi wa kutumia Mtandao wa Mambo, programu za Mtandao wa Mambo, Miji na Jamii za kidijitali; Mahitaji, uwezo, na muundo wa kiufundi katika sekta zote zinazohusisha Mtandao wa Mambo, ikiwa ni pamoja na kilimo, usafiri, fedha, huduma za umma, na mazingira; Miundo ya Mtandao wa Mambo na Miji na Jamii za kidijitali, itifaki, ubora wa huduma, na ubora wa uzoefu; Takwimu za uchambuzi, kushirikiana, uchakataji, na usimamizi, pamoja na vipengele vya data kubwa katika Mtandao wa Mambo na Miji na Jamii za kidijitali; Utafiti wa teknolojia za kidijitali zinazoibuka, lugha, na ufafanuzi na Uthamanishaji na tathmini ya miji na jamii za kidijitali endelevu,” alibainisha na kuongeza.    

Viwango vitakavyoafikiwa na ITU -T SG20 vitaiwezesha ITU kutoa mwongozo ili nchi wanachama wavitumie viwango hivyo katika mifumo ya miji na jamii zilizostaarabishwa na teknolojia za kidijitali.

ITU -T SG20 inajumuisha wawakilishi na wataalamu wa sekta ya umma na binafsi kutoka kote duniani, ukiwaleta pamoja wajumbe zaidi ya 300 wanaowakilisha serikali, sekta ya viwanda, wanataaluma, na taasisi za utafiti. Katika mkutano huo aidha Tanzania imepata fursa ya uwakilishi wa wataalamu kutoka serikalini, watoa huduma za mawasiliano ya simu (MNOs), watoa huduma za mtandao (ISPs), Mamlaka za udhibiti, na wanataaluma.

Awali akizungumza katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano huo, Idara ya Viwango vya Mawasiliano-pepe (Telecommunication Standardization Bureau - TSB) Bwana Seizo Onoe alisema: "Mtandao wa Mambo, Miji na Jamii za Kidijitali/maridadi ina uwezo wa kubadilisha maisha yetu na jamii kuwa bora zaidi. Lakini hili litaweza kutokea tu, ikiwa tunavyo viwango sahihi na mahsusi; hivyo ITU -T SG20 ina jukumu muhimu katika kukuza viwango hivi na kuhakikisha kuwa vinakubaliwa na kutekelezwa ulimwenguni kote."

Pia, wakati wa ufunguzi wa vikao vya jukwaa hilo, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania Mhandisi Kundo Mathew aliweka bayana kuwa Tanzania haitasalia nyuma kutumia mapema teknolojia zinazojadiliwa kwenye Mkutano huo akibainisha kuwa tayari Serikali imeubainisha Dodoma kuwa mji wa mfano kama mji maridadi/mji wa Kidijitali, huku Meya wa jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe akibainisha kuwa tayari jiji hilo, makao makuu ya Tanzania limefanya matayarisho yote muhimu kuufanya Dodoma mji wa mfano kama ‘smart city’.

Mkutano huo utahitimishwa Septemba 22, 2023, kwa wataalamu hao kufikia muafaka wa masuala yaliyojadiliwa.

Wataalamu wa Mawasiliano kutoka kote ulimwenguni wakijadili viwango vya miji na jamii za kidijitali na Mtandao wa Mambo jijini Arusha, Tanzania. Mkutano huo, unaoongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU), unafanyika kwa wiki mbili na unajumuisha wataalamu kutoka sekta za umma na binafsi. Viwango vinavyojadiliwa vinakusudiwa kuhakikisha kuwa miji na jamii za kidijitali ni salama, endelevu, na zinafaa kwa wote. PICHA: Mpiga Picha Wetu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...