Na Karama Kenyunko - Michuzi TV. 

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amemuagiza katibu Tawala  wa Wilaya hiyo, Charangwa Makwiro kumuandikia barua  Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha shule zote za msingi na sekondari zinaunda klabu za kodi ili kuelimishana kuhusu ulipaji wa kodi.

Amesema ni lazima wanafunzi waanze kujifunza  umuhimu wa kulipa kodi na kuhamasisha mahusiano mazuri kati ya mlipakodi, mfanyabiashara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na serikali.

Mpogolo ameyasema hayo leo Septemba 27, 2023 katika Shule ya Msingi Jamhuri, Dar es Salaam katika kampeni ya kuelimisha watanzania kuhusu matumizi sahihi ya  mashine za kielektroniki za EFD.

Amesema klabu hizo zitakuwa chini yake na kwamba yeye  ndio atakuwa mlezi kuhakikisha klabu hizo zinakuwa kama zile za rushwa na lishe.

Shule nyingine zilizoshiriki katika kampeni hiyo ni Shule za Sekondari Azania, Jamhuri, Dar es Salaam, Zawadi,  Gerezani, Pugu, Migombani, Benjamini, llala na Uhuru.

Ameeleza kuwa shule hizo zikiwa na klabu za kodi zitaona umuhimu wa kodi kama sehemu ya maendeleo na hivyo, watahamasisha wazazi kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.

Mpogolo amesema TRA walikuja na mashine hizo kwani ni kifaa kitumikacho kukusanya kodi na kwamba hakina udanganyifu endapo kitatumika kutolea risiti baada ya manunuzi.

Amesema zipo risiti feki au zenye tarehe za nyuma zinazotolewa na mashine ambazo sio  sahihi na husababisha mapato kupotea.

"Wiki inalenga kujenga mahusiano kati ya wakala namba moja wa serikali na mfanyabiashara ambaye ni wakala namba mbili. TRA na Wafanyabiashara sio maadui ndio maana tunawapatia mashine za EFD," amesisitiza Mpogolo.

Pia amesema "ukiona mfanyabiashara anakwepa kutoa risiti kwa kutumia mashine hiyo anakosa sofa ya uzalendo lakini pia mtumishi wa TRA akiomba rushwa katika kodi, anakosa sifa hizi," 

Ameeleza kuwa hakuna vita kati ya wafanyabiashara na TRA na lengo lao ni kuelimishana kwani masuala ya kodi na watoza ushuru yalikuwepo tangu zamani hivyo, hakuna sababu ya kugombana.

Amefafanua kuwa wananchi hulipa kodi kwa wafanyabiashara ambazo huipeleka serikalini na kisha kutumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi ikiwemo elimu bure ambapo Wilaya hiyo inapokea zaidi ya Sh bilioni 44.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...