Na Albano Midelo,Songea

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imedhamiria kuona idadi ya
faru Weusi inaongezeka kwa asilimia tano kila mwaka.
Mratibu wa Faru kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Philibert Ngoti
amesema hadi kufikia Aprili 2023,idadi ya faru nchini ilifikia 238 hivyo
kuvuka lengo la mpango wa Taifa wa kuongeza faru Weusi ambalo lilikuwa
ni faru 205 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023.

“Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1970 hadi 1980 Tanzania ilikuwa na faru
Weusi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa nchini waliofikia 10,000 hivyo
Tanzania ilijulikana kama nchi yenye faru wengi barani Afrika’’,alisema
Ngoti.

Hata hivyo alisema mwanzoni mwa miaka ya 1980 hadi 1990 idadi ya faru
ilipungua na kuwa chini ya 100,kutokana na uwindaji haramu na kwamba
upungufu wa faru pia ulitokea katika nchi zote zenye faru barani Afrika.

Amesema kutokana na hali hiyo faru Weusi waliwekwa kwenye kundi la
Wanyama walio hatarini kutoweka duniani na kwamba mwaka 1993 serikali
ya Tanzania ilikuja na toleo la kwanza la mpango wa Taifa wa miaka mitano
la uhifadhi wa faru Weusi.

Mratibu huyo wa Faru Taifa amesisitiza kuwa ,Wizara ya Maliasili na Utalii
imeendelea kuunda sera na mipango ya usimamizi na uhifadhi wa faru
Weusi na kwamba mpango huo unaoanzia mwaka 2019 hadi 2023 hivi
upo katika toleo la nne.

Amebainisha zaidi kuwa Mpango wa Taifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa
Faru Weusi wa mwaka 2019 hadi 2023 unahimiza kuja na mazao ya utalii
kwa kutumia faru Weusi waliopo.

Kulingana na Mratibu huyo,kuna aina tano za faru duniani kati ya hizo faru
weupe wapo wa aina tatu ambao wanapatikana katika bara la Asia na aina
mbili za faru Weusi wanapatikana katika bara la Afrika.

“Nchini kwetu tuna faru Weusi pekee ambao wamegawanyika katika aina
mbili ambazo ni faru Weusi wa mashariki na faru Weusi wa kusini kati,faru
mweusi aina ya kusini kati anapatikana kusini mwa Tanzania ukiwemo
Mkoa wa Ruvuma’’,alisema Ngoti.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas
amewaagiza wadau wa utalii kuhakikisha wanaendelea kuwahifadhi
Wanyama faru ambao wapo katika hatari ya kutoweka kutokana na
vitendo vya majangili na watu wote wenye nia ovu dhidi ya Wanyama hao.

Amesisitiza kuboreshwa kwa uhifadhi wa Wanyama hao kutasaidia
kuendelea kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwepo kwa faida ya kizazi cha
sasa na kijacho.

Ametoa rai kwa wadau wa maendeleo wakiwemo WWF,GIZ na PALMS
kuona umuhimu wa kuanzishwa bustani ya faru katika wilaya ya
Namtumbo kwa kuwa tayari eneo ambalo faru Weusi waliwahi kuishi
limeainishwa.

Faru mweusi ni mnyama mwenye pembe mbili ,ana uzito wa kilo kati ya
700 hadi 1,500,urefu mita 3.5,ni mnyama mwenye hasira na huwa
hatabiriki.

Ni vema mataifa yote ambayo yamebakiwa na faru kushirikiana
kuwahifadhi na kuwalinda wanyama hao adimu ambao wapo katika hatari
ya kutoweka katika uso wa Dunia.
 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza baada ya kuzindua Mkakati wa Utalii Mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea
Mratibu wa Faru Taifa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Philbert Ngoti akizungumza akitoa taarifa ya faru waliopo nchini na mipango ya serikali kuongeza idadi ya faruMichuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...