Na Mwandishi wetu Mtwara

Naibu Waziri; Wizara ya Nishati, Mhe. Judith Kapinga, tarehe 22 Septemba, 2023 amewasha umeme kwenye vijiji vinne (4) vilivyopo katika Jimbo la Ndanda na Masasi; vijiji hivyo vimepata umeme kupitia Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili) ambapo, imeelezwa thamani ya Mradi huo kwa mkoa mzima wa Mtwara ni shilingi bilioni 97.

Vijiji vilivyowashwa umeme katika siku ya kwanza ya ziara yake ni pamoja na kijiji cha Mpanyani na Msikisi, vilivyopo katika Jimbo la Ndanda na kijiji cha Chakama na Namikunda; vilivyopo katika Jimbo la Masasi.

Akizungumza katika kijiji cha kwanza cha Mpanyani, kilichopo katika Jimbo la Ndanda, alichokitembelea na kuwasha umeme kwa mara ya kwanza; Mhe. Judith Kapinga, amesema Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuanzisha na kuendeleza miradi ya nishati ya umeme vijijini na kusisitiza kuwa Wananchi wanapaswa kutumia fursa ya uwepo wa miradi hiyo hiyo kwa kuanzisha shughuli za maendeleo na kujiajiri.

Naibu Waziri Kapinga ameongeza kuwa ni vyema, Wananchi wakachangamkia fursa za uwepo wa Wakandarasi kwenye maeneo mbali mbali ya miradi na wakati huu ambapo zoezi la kuwasha vijiji likiwa linaendelea ili wajiunganishie na huduma ya umeme (Wiring) kwa kuwa gharama yake ipo chini ambayo ni shilingi 27,000 (Elfu Ishirini na Saba tu).

“Niwaombe na niwahamasishe kutumia fursa ya uwepo wa Wakandarasi kwenye maeneo miradi kwa kujiunganishia huduma ya umeme kwa kuwa Serikali imelipia huduma hiyo na mtaipata kwa shilingi elfu ishirini na saba tu (27,000/=); Wakandarasi wakishaondoka, eneo la Mradi (Site), gharama itakuwa kubwa na hamtaipata kwa bei hiyo”. Alisema Naibu Waziri Judith Kapinga.

Akiwa katika kijiji cha Namikunda; Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeamua kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote vya mkoa wa Mtwara, ambapo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) uliongezewa bajeti ambayo imewezesha kuongeza kazi kwa Wakandarasi katika vijiji 112 vya mkoa wa Mtwara, vijiji ambavyo awali havikuwa vimejumuishwa katika wigo wa awali na hivyo kufikia jumla ya vijiji 276 katika wigo wa kazi.

“Kutokana na uhitaji mkubwa wa kuwafikia Wateja wengi zaidi, Wakala uliongeza kilomita 2 za umeme wa msongo mdogo na wateja 42 kila kijiji kwa jumla ya vijiji 276 vijivyopo katika fungu 20 la Mradi wa REA III, Mzunguko wa Pili”. Alisema, Mhe. Judith Kapinga.

Naibu Waziri Kapinga, amemalizia kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa Miradi hiyo yote kwa mkoa wa Mtwara una wastani wa asilimia 60 za utekelezaji na kwamba Serikali itaendelea kuongeza wigo wa utoaji wa huduma hiyo kwa kadri fursa ya kufanya hivyo itakapopatikana.

Mhe. Judith Kapinga anaendelea na ziara yake katika mkoa wa Mtwara ambapo anatarajiwa kitembelea na kuwasha umeme kwenye vijijini vitatu vilivyopo katika Halmashauri ya mji mdogo wa Nanyamba na Jimbo la Nanyamba; vijiji hivyo ni pamoja na kijiji cha Nachuma, Kiwengulo na Mchanje


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...