Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WASIMAMIZI wa vituo vya uchaguzi mdogo wa Diwani Kata ya Nala, wametakiwa kufanya kazi kwa nidhamu, hekima na uzalendo na kuepuka kuisababishia serikali hasara.

Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini, John Kayombo alipokuwa akifungua mafunzo kwa wasimamizi wakuu na wasimamizi wasaidizi kwenye vituo vya uchaguzi mdogo wa Diwani Kata ya Nala, Jimbo la Dodoma mjini yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kayombo ambae ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “niwaombe sana wasimamizi wa vituo, uchaguzi ni suala nyeti sana sikiliza kwa makini maelekezo ya viongozi na fuata taratibu na sheria zilizopo, ukikosea utaitia serikali katika hasara kubwa. Kuweni na nidhamu, hekima na uzalendo kwa kiwango cha juu sana. Baadhi yenu mlishasimamia chaguzi nyingi ila uchaguzi hauhitaji mazoea. Tusiweke mazoea katika suala la uchaguzi”.

Alisema kuwa matarajio ni uchaguzi huo kufanyika vizuri na kumalizika salama. “Ninyi mmeaminika miongoni mwa watanzania wengi. Fanyeni kazi hii kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwa kushirikiana na wenzenu kama timu moja ili tumalize salama zoezi lililopo mbele yetu salama. Kama unajisikia huwezi kufanya kazi hii tuambie mapema upumzike” alisema Kayombo.

Kwa upande wake Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Mwanaisha Kwariko aliwapongeza wasimamizi hao kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kati ya wengi walioomba. 

“Lazima uheshimu hiyo dhamana uliyopewa kwa kufanya kazi hiyo kwa uaminifu. Niwaase kufuata sheria, kanuni na taratibu na miongozo kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kama kuna jambo limekutatiza uliza” alisema Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Kwariko.

Aidha, aliwataka kuheshimu kiapo chao cha kutunza siri na kuwaeleza kuwa kukiuka kiapo hicho wanaweza kushitakiwa kwa sheria husika. 

“Msiwe mashabiki wa vyama vya siasa, mmeshaapa kujitoa kwenye vyama vya siasa. Mnatakiwa kuhudumia watu wote kwa usawa” alisisitiza Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Mwanaisha Kwariko.

Akielezea sifa za wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo, Mratibu wa Uchaguzi, Albert Kasoga alisema ni lazima awe raia wa Tanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea. 

Sifa nyingine alizitaja kuwa ni uadilifu na utiifu mwenye akili timamu. 

“Hatakiwi kuwa shabiki au kiongozi wa chama chochote cha siasa. Awe amehitimu elimu ya kidato cha Nne au zaidi na anaweza kusoma na kuandika vizuri na anaweza kuelewa vizuri maelekezo ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura” alisema Kasoga. 

Uchaguzi mdogo wa Kata ya Nala unatarajia kufanyika tarehe 19 Septemba, 2023.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...