*Rais aipa kongole TCRA kwa ushiriki wake kama mbia wa mradi.

Na Mwandishi Wetu Arusha, 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua jengo refu zaidi jijini Arusha, ambalo sasa ni Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU).

Katika hafla hiyo muhimu, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa jengo hilo katika kukuza sekta ya posta barani Afrika, akisema ni tukio la kihistoria kwa Afrika. Alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na PAPU kwa ushirikiano wao imara uliosaidia kufanikisha mradi huu wa kuvutia.

"Nawapongeza sana TCRA na PAPU kwa kukamilisha mradi huu mkubwa," Rais Samia alisema. "Jengo hili litasaidia kukuza sekta ya posta barani Afrika na kuboresha huduma kwa wananchi."

Jengo la PAPU Tower lina ghorofa 17, limegharimu Billion shilingi bilioni 54.86. ambapo asilimia 60 ya gharama hizi zimetolewa na PAPU, huku asilimia 40 nyingine zikitolewa na TCRA kama mbia wa mradi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.

Katika hafla hiyo ya kihistoria, Rais Samia pia alizindua stempu mbalimbali zilizotolewa na Mashirika ya Posta wanachama wa PAPU, ambazo zinaonesha picha ya jengo hili lenye muonekano wa kipekee ambazo zitatumiwa kote Duniani katika shughuli za kila siku za kiposta.

Jengo la PAPU Tower lilianza kujengwa mwaka 2019 na kukamilika mwaka 2023. Ujenzi wa jengo hilo ulisimamiwa na kampuni ya ujenzi ya China State Construction Engineering Corporation, huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ikisimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ambao umependezesha mandhari ya jiji la Arusha.

Kabla ya tarehe ya uzinduzi, kulifanyika mikutano muhimu kujadili na kuweka mikakati ya kufanikisha mradi huu wa kuvutia na kuboresha sekta ya Posta Afrika. Mikutano hii ilihudhuriwa na viongozi na wanachama wa PAPU, Serikali ya Tanzania, pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Posta na Watendaji Wakuu wa Mamlaka za Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano. Walijadili namna nchi wanachama zinavyoweza kuondoa vikwazo vinavyosababisha kusuasua kwa ukuaji wa haraka wa sekta ya Posta barani Afrika.

Uzinduzi wa jengo la PAPU Tower unaashiria ushirikiano na maendeleo katika eneo la posta barani Afrika. "Jengo hili litasaidia kuboresha huduma za posta kwa wananchi wa Afrika na litaimarisha ushirikiano wa kimataifa, huku Tanzania ikiendelea kujijengea sifa ya kimataifa," alieleza Oyuke Phoustine, Afisa Habari wa PAPU

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabiri Bakari, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi kama ishara ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), lililojengwa kwa ushirikiano wa Tanzania kupitia TCRA na PAPU eneo la Sekei, Arusha.  Uzinduzi ulifanyika Jumamosi Septemba 2, 2023.

Sehemu ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) wakifuatilia kwa makini matukio ya uzinduzi. Jengo hilo limejengwa na kukamilika katika eneo la Sekei, Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali na Umoja wa Posta Afrika (PAPU), muda mfupi baada ya kukamilisha uwekaji wa jiwe la msingi kuzindua jengo la makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) lililopo eneo la Sekei, Arusha. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso (Mb), Mhe. Dkt. Khalid S. Mohamed - Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano, na Uchukuzi (SMZ), Mhe. Nape Moses Nnauye - Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari (WHMTH), JMT, Bw. Sifundo Chief Moyo - Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Dkt. Beaula Chirume - Katibu Mkuu Wizara ya Tehama, Posta, na Huduma za Vifurushi ya Jamhuri ya Zimbabwe, na Bw. Mohammed Khamis Abdulla - Katibu Mkuu WHMTH.
Viongozi mbalimbali wakipiga makofi kufurahia uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika lililozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Arusha. Jengo hilo limejengwa kwa ubia wa Serikali kupitia TCRA na PAPU kwa uwiano wa 60:40. Anaeonekana akifunua pazia kwenye jiwe la Msingi pamoja na Mhe. Rais ni Mtendaji Mkuu wa PAPU Bw. Chifundo Moyo. Picha: Hisani.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...