Said Mwishehe, Michuzi TV

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan  amesisitiza dhamira ya nchi yake ya kuleta mapinduzi katika sekta yake ya kilimo na kuibuka kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula barani Afrika.

Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia wajumbe zaidi ya 5000 kutoka mataifa mbalimbali waliohudhuria Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) mwaka 2023 unaoendelea jijini Dar es Salaam.

"Ninaamini kuwa Afrika inaweza kulisha dunia na serikali yangu imeongeza bajeti ya kilimo karibu mara nne, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kutoka dola za Marekani milioni 120 mwaka 2021/2022 hadi dola milioni 400 mwaka 2023/24 katika jitihada za kuchochea kilimo na mageuzi ya mfumo wa chakula nchini Tanzania,” amesema Rais Samia.

Aidha amewataka viongozi wa Afrika kuendana na Azimio la Malabo ambalo linayaamuru mataifa ya Afrika kutenga kima cha chini cha asilimia 10 ya bajeti zao kwa kilimo, ikilenga angalau asilimia sita kwa kiwango cha ukuaji wa kila mwaka.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Kikundi cha Washirika wa AGRF Hailemariam Dessalegn amezungumzia masuala muhimu yanayokabili Mifumo ya Chakula ya Afrika.

Ametaja baadhi ya masuala yanayokabili mfumo wa chakula ni na mzozo unaoendelea wa Urusi na Ukraine, athari mbaya za janga la COVID-19, kuongezeka kwa ukame na mafuriko, usumbufu wa usambazaji,migogoro, na masuala mengine muhimu.

"Tuko katika harakati za kupona kutokana na mishtuko mitatu mikuu na hitaji la kuchukua hatua za kuleta mabadiliko halijawahi kuwa la dharura zaidi. 

"Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika 2023 ni wakati mahususi wa kuangazia na kufungua ahadi za bara hili za kisiasa, kisera na kifedha na ubunifu kuelekea kufikia mifumo yenye tija, yenye lishe, shirikishi, thabiti na endelevu ya chakula barani Afrika,” amesema.

Katika mkutano huo pia ulishirikisha  wahudhuriaji wengine mashuhuri akiwemo Waziri Mkuu Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Benin Lionel Zinsou, Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa Nigeria Jonathan Goodluck pamoja na Waziri Mkuu wa zamani wa Guinea  Mohamed Beavogui.

Kuhusu Jukwaa la Mifumo ya Chakula la Afrika ndilo jukwaa kuu la dunia kuhusu kilimo na mifumo ya chakula barani Afrika, ambalo limewakutanisha wadau kuchukua hatua kwa vitendo na kushiriki majadiliano yatakayosogeza mifumo ya chakula ya kiafrika.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...