Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeweka historia kwa kufadhili mradi wa umeme wa maji wa Ijangala kuingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuwanufaisha zaidi wa wananchi 4,500 wa vijiji nane vya wilayani Makete.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd; kampuni inayomiliki Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala, Bwana Elikana Kitahenga, amesema tayari mchakato wa kuingizwa kwenye gridi umeanza rasmi baada ya kukamilika ujenzi wa kituo hicho.

Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala kwa sasa una uwezo wa kuzalisha KiloWati 360 ambapo kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa maana yake ni kuwa kampuni ya Nishati Lutherani (DKK) Investment Ltd itaanza kuuza umeme huo kwa Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO).

Akiongea na Wanahabari; Mkurugenzi Mkuu, Bwana Kitahenga amesema REA imetoa zaidi ya millioni 900 kwa awamu tatu katika kufadhili ujenzi wa mradi huo.

Amesema kukamilika kwa hatua hii ya kuanza kuingia Mradi wa Ijangala kwenye Gridi ya Taifa; kumetokana na uwezeshaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo mwaka 2013, Mradi huo ulipokea awamu ya kwanza, shilingi milioni 133 na baadae mwaka 2016 Mradi ulipokea shilingi milioni 426 na awamu ya tatu, wanataraji kupokea shilingi milioni 437.

Amesema mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa vijiji vya Masisiwe, Tandala, Ikonda, Usagatikwa na Ihela kwa kupata umeme wa uhakika utatokana na Mradi wa chanzo cha maji wa Ijangala.

Akieleza kuhusu tukio la kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa; Mshauri Elekezi wa Mradi huo wa Ijangala Prof. Zakaria Katambala kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) amesema kazi imefanywa vizuri na Wakandarasi wanne na kuongeza kuwa zoezi la kuunganisha Kituo hicho na Gridi ya Taifa litakamilika ndani ya wiki moja.

Amezitaja kazi zilizofanywa na Wakandarasi hao wanne, kuwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa linalokinga maji kutoka juu kuja chini ulipo Mradi (Power House); kazi nyingine ni ujenzi wa bomba la kusafirisha maji (Penstock) kutoka juu kuja chini kwenye mtambo wa kufua na kuzalisha umeme; kazi ya tatu ni ujenzi wa sehemu ya kuzalisha umeme (Power House) na sehemu ya mwisho ni ujenzi wa mfumo wa kuunganisha mtambo wa umeme wa chanzo cha maji ili uungane na umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

“Kazi imefanyika vizuri, na Wawakilishi wa TANESCO wapo eneo la Mradi ili kuangalia ubora wa kazi yetu na kujiridhisha, waturuhusu kuanza kuingiza umeme unaozalishwa hapa kuingia kwenye Gridi ya Taifa”. Alisema Profesa Katambala.

Akizungumzia kuhusu zoezi hilo la kuingiza umeme unaozalishwa na Mradi wa Umeme unaotokana na chanzo cha maji wa Ijangala kuingia kwenye Gridi ya Taifa; Mkurugenzi Mkuu, Bwana Kitahenga amesema zoezi hilo linataraji kushirikisha Wataalam kutoka REA, TANESCO na Mkandarasi aliyejenga njia ya umeme kuja kwenye chanzo cha kuzalisha umeme cha Ijangala; kampuni ya SILO Power na kuongeza kuwa linataraji kuendelea kwa wiki mbili hadi tatu, kuanzia Tarehe 5 Septemba, 2023.

Sehemu ya nje ya eneo ulipo Mradi wa kufua umeme kwa maji wa Ijangala, katika kijiji cha Masisiwe, Halmashauri ya wilaya ya Makete, Njombe; Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewezesha zaidi ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya ununuzi wa mashine za kufua umeme ambapo, jitihada hizo zimefanikisha kuanza kwa taratibu za kuiingizwa kwenye gridi ya taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd, Elikana Kitahenga (kulia) akitoa taarifa ya Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Ijangala mbele ya Wanahabari eneo la Mradi huo katika kijiji cha Masisiwe, Halmashauri ya wilaya ya Makete, Njombe
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd, Elikana Kitahenga (kulia) akimskiliza Mshauri Elekezi wa Mradi wa kufua umeme wa Ijangala, Prof. Zakaria Katambala kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) namna mashine za kuzalisha umeme zinavyofanya kazi katika kinu cha kuzalisha umeme, eneo la Mradi huo katika kijiji cha Masisiwe, Halmashauri ya wilaya ya Makete, Njombe
Sehemu ya kuongoza na mitambo ya kufua umeme katika kinu cha kuzalisha umeme, eneo la Mradi huo katika kijiji cha Masisiwe, Halmashauri ya wilaya ya Makete, Njombe


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...