MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Rehema Sombi, ameeleza namna ambavyo sera za mwelekeo wa CCM 2020-2030 zilivyolenga kusaidia vikundi vya kijamii wakiwemo vijana.

Rehema ameyasema hayo leo Septemba 25, 2023 katika kikao kilichoambatana na hafla ya kampeni ya uwekaji wa bendera ya malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals - SDGs) iliyofanyika katika jengo la Umoja House - Ubalozi wa Netherlands.

Aidha, amesema kuwa Chama kimeendelea kuisimamia serikali kuchukua hatua za kujenga ustawi na maendeleo ya jamii kwa kuimarisha huduma kwa makundi maalumu likiwemo la watu wenye ulemavu, vijana, watoto, wanawake na wazee.

Ametaja baadhi ya hatua hizo ni kuendelea kutoa ruzuku kwa taasisi za watu wenye ulemavu kila mwaka na kutoa vitendea kazi, pamoja na kuanzisha mfuko maalumu wa watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.

“Hatua nyingine ni kutekeleza Sera ya jinsia ya mwaka 2016 ambayo inatoa mwongozo wa kusimamia masuala yote ya wanawake nchini, kuanzisha mtandao wa wajasiriamali wanawake na kutekeleza mpango kazi wa miaka mitano wa kupambana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto (2017 - 2022),” amesema.

Pia, ametaja hatua nyingine ni kutoa mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana 79,675 na kuviwezesha vikundi vya vijana 796 vinavyojishughulisha na kilimo, ufugaji na ushoni kupata mikopo kupitia mfuko wa uwezeshaji hivyo kufanikiwa kujiajiri katika maeneo ya kilimo.

Pamoja na hayo ameonyesha msimamo wa serikali katika kuweka mkazo juu ya masuala ya elimu hususani ya sayansi kwa wasichana.

Pia, makamu mwenyekiti huyo ameeleza namna serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyoweka juhudi kubwa kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu hususan kupitia ujenzi wa miundombinu wezeshi ya kimaendeleo na kushirikisha vijana katika ukuzaji uchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mkutano huo umeongozwa na Balozi wa Netherlands nchini Tanzania Wiebe De Boer ambaye amesisitiza kuwa vijana ndilo kundi muhimu kwa mabadiliko ya maendeleo kwa nchi yao.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...