Na. WAF - Dodoma 

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana na wadau wa huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa kuimarisha huduma za uchunguzi wa maabara, Vifaa-Tiba, damu salama pamoja na ubora wa huduma ili kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu. 

Hayo ameyasema leo Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi Dkt. Alex Magesa wakati akifungua mkutano wa kitengo cha huduma za uchunguzi wa magonjwa pamoja na wadau wa huduma za uchunguzi wa magonjwa kilichofanyika Jijini Dodoma. 

“Tunaendelea kushirikiana na wadau hawa ili kuondoa kero kwa wananchi ambapo miongoni mwa kero hizo ni pamoja na upatikanaji wa Vitendanishi, Vifaa, Vifaa-Tiba ikiwemo ya mionzi na upande wa damu salama”, amesema Dkt. Magesa.

Amesema, ili kufanikisha hayo lazima kazi ifanyike Kama timu ambapo kikao hicho kikimalizika wajumbe wataondoka na maazimio ambayo yatawezesha kwa kila mmoja kujua majukumu yake na anasaidiaje katika kufikia malengo makuu ya Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla. 

“Lengo la mkutano huo ni kuwasiliana na kujadili vipaumbele vya huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa wadau wote ili kuweka mikakati ya pamoja ya kufikia malengo ya Wizara ya Afya katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa”. Amesema Dkt. Magesa.

Aidha, Dkt. Magesa amesema, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alitoa malengo mbalimbali ambayo yanatakiwa kutekelezwa kwa wakati ili kutatua kero za wananchi ndio maana wameamua kuitisha nguvu ya pamoja ikiwemo nguvu za wadau. 

“Katika kutekeleza malengo aliyoyatoa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ndio maana tumeamua kukutana ili tuweze kujadiliana namna ya kutekeleza maelekezo hayo ili tuweze kuwahudumia wananchi kwa urahisi na haraka”. Amesema Dkt. Magesa.

Pia, amesema kwenye mashirikiano hayo yatawezesha kusongesha gurudumu la maendeleo katika upande wa uchunguzi na kutoa huduma zilizo bora ili kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

“Lakini pia mashirikiano haya yatawezesha kupatikana kwa wakati takwimu sahihi ili kuhakikisha tunaleta huduma za uchunguzi wa haraka kwa wananchi na wananchi wafurahiye matunda ya uwekezaji kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia na Waziri wetu Mhe. Ummy Mwalimu (MB)”. Amesema Dkt. Magesa.

Mwisho, Dkt. Magesa amesema bila uchunguzi Idara ya uchunguzi hakuna huduma za tiba ambazo zitaendelea nchini hivyo mategemeo ni kwamba uchunguzi bora unatoa matibabu bora kwa wananchi


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...