SERIKALI kupitia kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya imesema kuwa ni kweli imeshasaini mkataba wa ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya kutoka Ifakara hadi Mbingu Mlimba yenye urefu wa km 62.5 na kwamba kinachosubiriwa ni mkandarasi kuanza kazi hiyo.

Naibu Waziri Kasekenya ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza sambamba na ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Kihansi Mlimba yenye urefu wa km 126.39.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kasekenya amesema mkataba baina ya Serikali na Mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Ifakara hadi Mbingu ulishasainiwa na kinachosubiriwa ni kumalizika kwa siku 28 za Mkandarasi kutoa dhamana ya utendaji kama sheria inavyotaka kisha baada ya hapo ataanza kazi hiyo.

" Ni kweli tumesaini mkataba na mkandarasi na kinachosubiriwa ni yeye atoe dhamana ya utendaji kama sheria inavyotaka kisha ataanza kazi. Na dhamana hiyo anatakiwa aitoe ndani ya siku 28. Lakini pia kuhusu ujenzi wa km 37.5 za kutoka Mbingu hadi Chita ili kukamilisha km 100 nazo muda siyo mrefu tutasaini mkataba na mkandarasi," Amesema Kasekenya.

Akijibu swali la Mbunge Kunambi kuhusu ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Kihansi Mlimba, Naibu Waziri Kasekenya amesema kiasi cha Sh Milioni 250 kimetengwa kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo na baada ya kukamilika kwa zoezi hilo na kujua gharama ya ujenzi Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...