Kazi na dawa! Mkuu wa wilaya ya Temeke Mhe. Mobhare Matinyi akiteta jambo na mfanyabiashara katika soko la Stereo, wilayani Temeke.

Mkuu wa wilaya ya Temeke Mhe. Mobhare Matinyi akisikiliza kwa makini kero na changamoto za wafanyabiashara wa soko la Stereo, wilayani Temeke.

Mkuu wa wilaya ya Temeke Mhe Mobhare Matinyi akishiriki vema shughuli ya usafi katika soko la stereo, wilayani Temeke.



 Na: Joanita Joseph

KATIKA muendelezo wa wiki ya usafi, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe.Mobhare Matinyi leo Septemba 13, 2023 ameungana na wananchi kufanya usafi katika masoko makubwa wilayani humo.

Akiongea katika mkutano wa hadhara na wafanyabiashara wa soko la Kisewe, lililopo kata ya Chamazi, Mhe Matinyi amesema kuwa zoezi la usafi linapaswa kuwa endelevu na kila mtu awajibike kwa manufaa ya kiafya na kimazingira kwa ujumla.

"Mwaka wa fedha uliopita Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliipatia wilaya ya  Temeke Tshs Bilioni 152 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo hospitali, shule, maji, umeme, masoko na barabara hivyo moja ya jukumu kubwa kwa sisi wananchi ni kuhakikisha tunaitunza kwa usafi, tunataka kuwa na Temeke safi inayong'ara" Alisema Mhe. Matinyi

Aidha wafanyabiashara katika soko hilo wametumia nafasi hiyo kuwasilisha changamoto zao ikiwemo barabara, mifereji pamoja na uboreshaji wa miundombinu ukizingatia kuwa soko hilo ni soko la tatu kufanikisha upatikanaji wa mapato wilayani humo.

Hata hivyo Mhe Matinyi amewahakikishia kuwa serikali inatarajia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ikiwemo mifereji  kwa awamu ya pili chini ya wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA).

Vilevile alibainisha kuwa Manispaa Temeke ina idadi ya masoko takribani 27 yanayoendelea kuboreshwa, hivyo utawekwa utaratibu mzuri na soko hilo liingie kwenye mpango wa kuboreshwa kwani ni kweli limekuwa tegemezi kubwa kwenye mapato katika manispaa hiyo.

Kwa upande wake Mhe. John Gama, diwani wa kata ya Chamazi amemshukuru Mkuu wa wilaya kwa ujio huo na ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya katani humo ikiwemo upatikanaji wa kituo cha afya Mkondogwa, Jengo la mama na mtoto na upasuaji kwa zahanati ya Mbande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...