Na Karama Kenyunko Michuzi TV

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema katika kipindi cha
miaka mitatu mfululizo, makusanyo ya kodi yameongezeka kutoka Sh trilioni 18.14 mwaka 2020/21 hadi Sh trilioni 24.13 mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 8.33.

Pia imesema makusanyo ya jumla ya kodi nchini yamepanda kutoka Sh. trilioni 6.87 mwaka 2020/21 hadi Sh trilioni 9.03 mwaka jana.

Naibu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Mcha Hassan Mcha ameyasema hayo Leo katika semina waliyoiandaa kwa walipa kodi wakubwa.

Amesema mchango wa wafanyabiashara hao unaonekana pia katika kuongeza ajira, vipato vya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

Mcha amesema ili kuongeza ari ya watu kulipa kodi kwa hiari, TRA imefanya maboresho ya mifumo na miundo ili kuwahudumia kwa haraka walipakodi wakubwa, wa kati na wadogo na kwamba kwenye idara ya walipakodi wakubwa, mamlaka hiyo imeanzisha divisheni ya ufundi ili kushughulikia kwa wakati mahitaji ya wateja.

Aidha, amesema itaendelea kuweka mifumo itakayowaunganisha wadau wa forodha ikiwamo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ili kurahisisha uondoshaji wa shehena bandarini na  bandari kavu kwa wakati.

“Tunaendelea kuboresha mfumo wa forodha kwa kuboresha moduli zilizopo pamoja na kujipanga moduli mpya ikiwa ni pamoja na smart gate, ili kupunguza usumbufu na muda unaotumika kwenye mageti ya bandari, bandari kavu na mipakani,” amesema Mcha.

Ameeleza kuwa  mfumo mwingine ni wa makadirio ya ushuru kielektroniki utakaochakata thamani ya mzigo na kutoa ushuru wa forodha katika bidhaa na ule wa biashara mtandaoni ili kurahisisha huduma kwa wanaosafirisha vifurushi kwa ndege.

“Tunaendelea kujenga mfumo wa dirisha moja wa uondoshaji wa shehena maeneo ya forodha unaolenga kuruhusu wadau wote wa biashara na wasafirishaji kuwasilisha mara moja taarifa na nyaraka za shehena zinazoingia na kutoka nchini…lengo ni kutoa ankara moja ya malipo ya kodi na huduma zote za uondoshaji wa mizigo bandarini,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mcha ameeleza  katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, TRA imerejesha kodi ambapo jumla ya sh. Bilioni 222.9, bilioni 995. 7 na Trilioni1.07 zimeidhinishwa na kulipwa na serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, 2022/2022 na 2022/2023.

Aidha amesema, TRA itaendelea kuhakikisha hakuna ucheleweshaji unaotokea katika uchakataji na ulipaji wa marejesho ya kodi…naomba niwakumbushe kuwasilisha ritani na makadirio ya kodi kwa wakati pamoja na kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka riba na adhabu,” amesema.

Pia amewataka walipakodi hao wakubwa kuendelea kutumia kwa usahihi mashine za risiti za kielektroniki (EFD), kuweka stempu za ushuru wa bidhaa, kulipa kodi kwa wakati na kuacha kutumia njia za panya kuingiza bidhaa nchini.

Baadhi ya wafanyabiashara waliiomba TRA kuimarisha mifumo yake ili waweze kuitumia kwa urahisi kupata huduma za kikodi.

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mcha Hassan Mcha, akizungumza wakati  Semina iliyoandaliwa na TRA kwa walipakodi wakubwa. Semin hiyo imefanyika leo Septemba 26,2023 jijjni Dar es Salaam.

 

Kamishna wa Walipakodi Wakubwa TRA, Alfred Mregi, akizungumza wakati  Semina iliyoandaliwa na TRA kwa walipakodi wakubwa. Semina hiyo imefanyika leo Septemba 26,2023 jijjni Dar es Salaam.
 

Sehemu ya walipa kodi wakubwa zaidi wakifuatilia semina hiyo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...