Na Said Mwishehe, Michuzi Blog

SHIRIKA la Reli Tanzania(TRC) pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani(WFP)wamezindua na kukabidhi mabehewa maalum matano yenye majokofu ambayo yatatumika kusafirisha matunda katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam.

Kuzinduliwa kwa mabahewa hayo yenye kuhifadhia matunda ili yasiharibike inakwenda kuondoa changamoto ya kuharibika kwa matunda wakati ya kusafirishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa kwa mabehewa hayo Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema  yatatumika kusafirisha bidhaa za matunda katika mikoa hiyo.

"Wakulima wa mazao hayo kama watatumia vizuri usafiri huo wa reli kutoka katika mikoa hiyo na  utawaongezea ufanisi kwenye kilimo chao na kuwaongezea kipato.Pia wafanyabiashara wa matunda na mbogamboga watakuwa na uhakika bidhaa zao ziko salama.

"Nitoe maagizo kwa TRC ihakikishe usafiri kutumia mabehewa haya uwe endelevu na wenye gharama rafiki kwa wakulima, lengo ni kusaidia wakulima wetu kusafirishia bidhaa zao kuja Dar es Salaam pasipo kuharibika na kupunguza hasara mkulima," amesema 

Prof.Mbarawa amesema Serikali inatambua mchango wa kilimo katika Taifa hili ndio maana imeendelea kutoa ushirikiano katika shughuli za kilimo ili kukuza pato la nchi kwa kiasi kikubwa zaidi na katika kuondoa changamoto za mazao kuharibika na gharama kubwa za usafirishaji.

Amefafanua kwa kukosa miundombinu rafiki ya kusafirisha na kuhifadhi mazao ya mbogamboga na matunda TRC ikishirikiana na WFP imekuja na mradi wa kuwasaidia wakulima kusafirisha mazao kwa njia rahisi zaidi kwa kutumia mabehewa yenye makasha yanayohifadhi ubaridi wa nyuzi joto 40.

Ameongeza Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeshirikiana na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda kuunga mkono jitihada zinazofanywa na TRC na WFP kuhakikisha upatikanaji wa masoko , miundombinu ya kuhifadhia mbogamboga na matunda pamoja na usafiri wa uhakika kwa gharama nafuu ili wakulima kunufaika na kuleta maendeleo katika nchi.

"Naomba niwahakikishie wadau wa kilimo na biashara kuwa Wizara ya Uchukuzi kupitia TRC itahakikisha wakulima na wafugaji wanapata huduma bora ya usafirishaji wa mazao yao kupitia usafiri wa reli kwa kutumia makasha haya yenye ubaridi, " amesema Waziri Mbarawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi na mwakilishi mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson, amesema kupatikana mabehewa hayo kutatoa fursa kwa mikoa ya Dodoma Morogoro na Dar es Salaam wakulima wake kuwa na uhakika wa kusafirishia bidhaa zao pasipo kuogopa kuharibika njiani kabla ya kufika sokoni.

Amesena WFP wanajivunia kufanikisha kupatikana kwa mabehewa hayo yaliyogharimu Sh.milioni 840 na kwamba wataendelea  kushirikiana na TRC na Serikali kwa ujumla kuweka mazingira mazuri kwa wakulima wa mbogamboga kutoka mikoa ya mbali na Dar es Salaam.

Sarah amesema Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji 20 wakubwa duniani wa mazao ya bustani yanayovunwa moja kwa moja kutoka shambani .Sekta ya kilimo cha bustani inakuwa kwa kasi zaidi na inaongozwa na wakulima wadogo na inawakilisha asilimia kubwa na muhimu ya pato la Taifa linalotokana na kilimo.

Amesema pamoja na maendeleo makubwa yaliyopatikana na umuhimu wa kilimo cha bustani kwa uchumi kiasi kikubwa cha mazao hayo kinachokadiriwa kuwa kati ya asilimia 30 hadi 40 hupotea  katika mnyororo wa thamani na sababu kubwa ni ukosefu wa hifadhi ya baridi.

Aidha amesema kwa kuzingatia mafanikio ya awamu ya awali WFP na TRC wanaweza kupanua mradi hadi sehemu za ziada za reli zikiwemo Arusha, Kilimanjaro,  Tanga hadi Dar es Salaam ambao unalenga kushughulikia jambo hilo la usafirishaji mazao ya bustani katika mikoa hiyo.

"WFP imekuwa ikiunganisha wakulima wadogo wadogo na masoko tangu mwaka 2009 .Mradi huu utatoa usafiri wa uhakika, salama na wa gharama nafuu kwa ajili ya mazao ya wazalishaji wadogo na wakusanyaji wa mazao kufika katika masoko."

Awali Mkurugenzi wa TRC, Amina Lumuli, amesema Shirika hilo litatanua huduma hiyo na kufikia mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa mingine yenye huduma ya usafiri wa reli na kwamba wameanza na mikoa mitatu.

 "Lengo ni kusambazwa huduma hii katika mikoa yote wanayozalisha mazao ya mbogamboga na matunda.Mabehewa hayo yana uwezo wa kubeba zaidi ya tani 200 ya mazao hayo ya mboga mboga na matunda."

Wakati huo huo Mwakilishi wa wadau wa mazao hayo Ally Mbuguyo amesema kuwepo kwa mabehewa hayo ni neema kwao kama wafanyabiashara wa mazao hayo na yataeqongezea tija kwenye biashara zao.
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makambe Mbarawa (katikati) akiwa na Mkurugenzi wa WFP Tanzania Sarah Gibson ( wa tatu kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa TRC ( wa nne kulia) pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja wakikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa mabehewa matano ya kusafirisha matunda na mbogamboga
Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua mabehewa matano ambayo yatatumika kusafirisha mazao ya matunda na mbogamboga kwa kutumia usafiri wa reli
Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa akizungumza na Mkurugenzi wa WFP Tanzania Sarah Gibson kabla ya kuzinduliwa kwa mabehewa ya kusafirisha mazao ya bustani kama mbogamboga.Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Sslaam
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania( TRC) Amina Lumuli akizungumza wakati wa hafla hiyo





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...