Na. Theresia Nkwanga, NALA

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini, John Kayombo amewataka wakazi wa Kata ya Nala kujitokeza na kutumia haki yao ya kidemokrasia kupiga kura kumchagua mwakilishi wao.

Kayombo alisema hayo katika kituo cha Sengu chini apokuwa akitoa muhtasari wa hali ya uchaguzi mdogo wa Diwani Kata ya Nala unaoendelea katika vituo 12 vya kata hiyo.

Leo tarehe 19 Septemba, 2023 Kata ya Nala inafanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya aliyekuwa Diwani aliyefariki. Zoezi la kufungua vituo lilifanyika kama sheria inavyotaka saa 1:00 asubuhi. Mpaka sasa saa 6 mchana zoezi la upigaji wa kura linaendelea vizuri na wananchi wamejitokeza kwa wingi kuja kuchagua mwakilishi wao. Niwaombe wananchi waendelee kujitokeza muda bado sasa ni saa 6 mchana hadi saa 10 jioni ndio tunafunga vituo” alisema Kayombo.

Aidha, aliwataka wananchi wakimaliza kupiga kura kurudi nyumbani. "Vituo vya kupiga kura baadae vinabadilika kuwa vituo vya kuhesabia kura. Mwisho matokeo ya kila kituo yatabandikwa kwenye mbao za matangazo kwa kila kituo. Baada ya zoezi hilo, wasimamizi wote wataondoka kuja kwenye kituo cha majumuisho ya vituo vyote kwenye Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Nala. Mshindi wa kiti cha Diwani Kata ya Nala atatangazwa leo na cheti cha ushindi kitatolewa leo” alisisitiza Kayombo.

Kuhusu hali ya upigaji kura, alisema kuwa wananchi wanapiga kura katika hali ya amani na utulivu. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imejipanga vizuri kabisa.

Kwa upande wake Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Mwanaisha Kwariko alisema kuwa hali ya vituo vya kupigia kuwa ni nzuri na vifaa vyote vilifika mapema na watendaji wote walikuwepo na ilipofika saa 1:00 asubuhi watendaji walikuwa tayari kuwapokea wapiga kura.

“Katika vituo vingi tulivyotembelea wapiga kura wengi walikuwa wameshafika kwa ajili ya zoezi hilo na wananchi walikuwa wakifuata maelekezo ya kujipanga kwenye mistari kwa ajili ya kupiga kura kwa utaratibu. Muitikio wa watu ni mzuri wa watu kishapiga kura wanaondoka. Hata wenye mahitaji maalum wanapokelewa na kuhudumiwa kama tulivyoelekeza wanapiga kura mapema na kuondoka” alisema Mhe. Kwariko.

Nae Mratibu wa Uchaguzi, Albert Kasoga alisema kuwa walijiaandaa vizuri kwa vituo vyote 12. “Kwa upande wa wasimamizi maandalizi yalifanyika na wote walipata mafunzo na wapo vizuri na wapo vituoni kama maelekezo yalivyokuwa” alisema Kasoga.

Mkazi wa Mtaa wa Chiwondo, Samwel Kusalo alisema kuwa zoezi hilo limeratibiwa vizuri. “Tulitangaziwa leo ni siku muhimu ya kutumia haki yetu ya msingi kupiga kura kumchagua diwani wetu. Nimekuja, nimepokelewa vizuri na wamekagua wakaona jina langu na nikatumia haki yangu ya msingi kupiga kura” alisema Kusalo.

Kata ya Nala yenye jumla ya wapiga kura 3,741 na vituo 12 vya kupigia kura inafanya uchaguzi mdogo kufuatilia kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo Julius Chimombo aliyefariki tarehe 10 Aprili, 2023 huku vyama vinavyoshiki uchaguzi huo vikiwa 11.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...