#Ni ya kwanza tangu uhuru;
Na Derek Murusuri, Mwanza
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeipongeza Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) kwa kuasisi andiko la rasimu ya Sera ya Huduma za Maktaba ya kwanza kabisa nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa sera hiyo itakuwa ya kwanza nchini, hivyo kuipongeza Bodi na Menejimenti ya TLSB kwa mafanikio hayo makubwa.
Prof. Nombo alitoa pongezi hizo katika hotuba yake ya kufungua Rasmi kongamano la tatu la kuboresha huduma za maktaba nchini, iliyosomwa kwa niaba yake na Bw. Victor Bwindiki, Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji Sera za Elimu Msingi, katika Wizara hiyo.
Alisema Sera hiyo, itakapokamilika, itasaidia kupanua wigo wa utoaji wa huduma za maktaba nchini, ikiwa ni pamoja na kujenga ari ya uandishi na kuhuisha utamaduni wa usomaji.
“Kipekee ninaomba niipongeze Bodi kwa mchango mchango muhimu katika kuwaelimisha watanzania kupitia machapisho mbali mbali,” alisema.
Aliipongezi TLSB kwa kuwajali watoto wenye mahitaji maalum kwa kuzindua huduma za maktaba kwa watoto kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (RRH) ya Sekou Toure ya jijini Mwanza.
Maktaba ni kitovu cha maarifa na inachangia kwa kiasi kikubwa kujenga jamii iliyoelimika.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Dkt. Mboni Ruzegea, aliiomba wizara kuwaongezea raslimali fedha na raslimali watu ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya huduma za maktaba nchini.
Alisema taasisi yake ina raslimali watu 287 wakati mahitaji halisi ni watumishi zaidi ya 1,000, lakini ikama ni wafanyakazi 400.
Akijibu ombi hilo, Bw. Bwindiki ameahidi kuyafikisha mahitaji ya TLSB kwa Katibu Mkuu ili kuona uwezekano wa kuyapatia ufumbuzi.
Kongamano hilo linalofanyika katika ukumbi wa chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza, linahudhuriwa na wakutubi, waandishi na wachapishaji wa vitabu kutoka hapa nchini.
Akiongea katika kongamano hilo, mwakilishi wa chama cha Wakutubi Tanzania (TLA), Bw. Barnabas Bwango, amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TLSB kwa maono makubwa ya kuiendeleza fani ya ukutubi na kuipa hadhi inayostahili nchini.
“Wasomaji wa vitabu, waandishi na wakutubi wote nchini tunapaswa kumuunga mkono na kumsaidia ili afikie malengo aliyoyakusudia,” alisema.
Hadi sasa, TLSB tayari imeshatoa mafunzo kwa wakutubi zaidi ya 8,000 kupitia chuo chake kilichopo Bagamoyo.
Akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Dkt. Grace Msoffe kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema utamaduni wa usomaji unajengwa katika miaka ya mwanzo ya mtoto.
Alionya kuwa utamaduni wa usomaji nchini umeshuka sana. Baadhi ya sababu ni kutokuwepo na maktaba za kutosha pamoja na machapisho.
“Hatuna maktaba kwenye shule zetu za msingi, sekondari, katika ofisi na sehemu nyingine za umma,” alisema Dkt. Msoffe.
Wakichangia mada kuhusu Sera ya Maktaba, iliyowasilishwa na Prof. Alfred Sife, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, washiriki waliitaka sera ielekeze kuwepo na maktaba katika ofisi zote za umma.
Prof. Sife alisema nchini Finland, wananchi wa kawaida hujaza maktaba zao, hata nyakati za kazi. Alisisitiza umuhimu wa kuhuisha utamaduni wa kujisomea.
Kongamano hilo linatarajiwa kufingwa kesho.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...