#Asisitiza Watanzania wanataka umeme
#Atoa Pongezi kwa wafanyakazi kwenye mradi huo
#TANESCO wapongezwa kwa hatua ya ujenzi
Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme wa Msongo wa kilovoti 400/220/132/33 wa kituo cha Chalinze umefikia asilimia 84.3 na hivyo kuleta matumaini ya kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme.

"kwa sasa ujenzi umefikia asilimia. 84.3 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 31 Disemba, 2023. Mradi huu unakwenda kupunguza changamoto ya umeme kwa kiasi kikubwa hususan katika mkoa huu wa Pwani," amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa, mara baada ya Mradi huo kukamilika, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea Megawatt 2115 kutoka katika Bwawa la kuzalisha Umeme wa Maji la Julius Nyerere na kitasambaza Megawati 850 kwenye mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani na kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa hiyo.
Akizungumza na wafanyakazi wanaofanya kazi katika mradi huo amewataka wafanye kazi kwa bidii kwa kuwa Serikali imewapa ushirikiano ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Meneja wa Mradi wa kituo hicho Mhandisi Newton Livingstone Mwakifwamba amesema kuwa Serikali imetoa ushirikiano mkubwa katika utekelezaji hususan katika mazingira mazuri ya wafanyakazi. Amesema mradi huo utakamilika kwa muda uliopangwa ifikapo mwezi Desemba 2023.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema toka kuanza kwa mradi huo hakuna changamoto iliyojitokeza kukwamisha mradi huo. Amempongeza Dkt. Biteko kwa kutembelea mradi huo kujionea maendeleo yake.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kuwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa mradi utakapokamilika utakua ni msaada mkubwa wa mkoa wa Pwani.
Mradi huo ulianza rasmi tarehe 6 Septemba, 2021 ambapo kazi za ujenzi zilianza tarehe 11 Oktoba, 2021 na unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze pamoja na kituo cha kupoza umeme na kusafirisha umeme kuelekea mikoa ya kaskazini kwa kuingizwa Kenya Gridi ya Taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...