Na Mwandishi Wetu, Mtwara
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema Serikali inatarajia kujenga Bandari mpya katika eneo la Kisiwa Mgao mkoani Mtwara.
Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa ziara yake Naibu Waziri Kihenzile amesema hayo jana Oktoba 4 wakati akikagua utendaji kazi wa Bandari na Kiwanja cha Ndege cha Mtwara.
Naibu Waziri Kihenzile amesema, bandari hiyo mpya itakuwa ni maalumu kwa ajili ya usafirishaji bidhaa zijulikanazo kama ‘bidhaa chafu’ ambazo ni kama makaa ya mawe na saruji.
Amesema wizara ina mipango ya muda mfupi na mrefu katika usimamizi na matumizi ya bandari ya Mtwara, hivyo moja ya mipango yao ni kujenga bandari mpya wa Kisiwa Mgao.
"Serikali inakwenda kujenga bandari nyingine mkoani Mtwara katika eneo linalofahamika kama Kisiwa Mgao ambapo kwa sasa hatua za manunuzi zimeanza," amesema.
Amesema Wizara ya Uchukuzi inaendelea kuweka mikakati ya namna ya kuimarisha bandari ya Mtwara, ili kuhakikisha bidhaa nyingine pia zinasafirishwa kwa wingi.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...