Asisitiza Wakuu wa mikoa, Wilaya kuwa wabunifu kutangaza  fursa za utaliii

Awahimiza Watendaji kutimiza wajibu wao kuwahudumia Watanzania

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko  amezindua mpango mkakati wa kutangaza fursa  zilizopo Sekta ya Utalii katika wilaya ya Pangani, mkoani Tanga  ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuikuza sekta hiyo nchini.

Dkt. Biteko amefanya uzinduzi huo Oktoba 7, 2023 jijini Dar es salaam katika Kongamano la Uwekezaji la Swahili International Tourism Expo lenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko katika wilaya hiyo ikiwemo utalii katika mbuga ya Saadani, fukwe, kilimo biashara pamoja na uchumi wa Buluu katika wilaya hiyo.

Vile vile, alisisitiza kuwa, Kongamano hilo litumike kuitangaza wilaya ya Pangani na kubadilishana mawasiliano ili fursa zilizoko Pangani ambazo hazipatikani kwengine zishawishi watu wengine kuzifuata.

"Niwapongeze sana watu wa Pangani kupitia Mkuu wa wilaya kwa ubunifu huu wa hali ya juu na nitoe wito kwa wilaya zingine kuiga Pangani na kufungua fursa za utalii na uwekezaji kwenye wilaya zao" Alisema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula alisema kuwa, sekta ya utalii kwa sasa mchango wake katika Pato la Taifa ni asilimia 17. Alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira rafiki katika sekta hiyo ili kuendelea kuvutia utalii nchini katika maeneo mbalimbali hususan wilaya ya Pangani.

Awali akizungumza kabla ya mgeni rasmi, Mkuu wa wilaya ya Pangani  Mhe. Zainabu Abdallah alisema, wilaya ya  Pangani imejikita kwenye uwekezaji wa maeneo matatu ikihusisha utalii , kilimo mkakati na uchumi wa bluu na kuongeza kuwa wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya ya kimkakati  yenye mazingira mazuri ya uwekezaji.

" Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na tunawaomba wawekezaji kufika wilaya ya pangani kujionea fursa hizo muhimu  "alisisitiza Mhe. Zainabu

Uzinduzi wa mpango huo ulikwenda sambamba na Kongamano la uwekezaji chini ya maonyesho ya wadau wa Sekta ya Utalii kuunga mkono fursa za uwekezaji.

Wengine walioshiriki hafla hiyo ni Viongozi mbalimbali wa Serikali, watendaji wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo na wadau wa sekta ndani na nje ya nchi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...