Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali itaendelea kutenga miradi ya ujenzi kwa ajili ya wakandarasi wanawake ili kuwawezesha wakandarasi hao kupata uzoefu, kukuza mitaji na kutoa fursa kwa Watanzania.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wakandarasi Wanawake jijini Dar es Salaam, Eng. Kasekenya amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakandarasi wanawake wanaimarika na kutekeleza miradi mingi ya Serikali ambayo inatekelezwa nchini.
“Chapeni kazi, pia kamilisheni miradi kwa wakati ili Serikali iwaamini na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kupata kazi nyingi zitakazowainua kiuchumi kama walivyo makandarasi wengine”, amesema Eng. Kasekenya.
Aidha, amewataka wakandarasi wanawake kuwa waaminifu na waadilifu ili kuaminiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi za kifedha na kuweza kupata mikopo kwa urahisi hatimaye kukuza mitaji yao.
Amezungumzia umuhimu wa Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kuwajengea uwezo wakandarasi wanawake ili wamudu kutekeleza miradi mbalimbali nchini ikiwemo miradi midogo na mikubwa.
“Awamu ya Sita imejipanga kutekeleza miradi mingi ya miundombinu hivyo unganeni jengeni uhusiano mzuri na taasisi mbalimbali ili mpate kazi,” amesema Kasekenya.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake, Eng, Judith Odunga, ameishukuru Serikali kwa namna inavyotoa vipaumbele vingi kwa wakandarasi wanawake na kusisitiza utaratibu huo ukiendelea uchumi kwa wakandarasi wanawake utakuwa na kuchochea maendeleo ya nchi.
Huu ni mkutano Mkuu wa Tatu kufanyika kwa wakandarasi wanawake, ambapo mkutano huu hufanyika mara moja kwa mwaka lengo likiwa ni kuwakutanisha pamoja, kujadili changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya
akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Wakandarasi wanawake uliofanyika katika
Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam leo Oktoba 12, 2023.
Baadhi ya wakandarasi wanawake wakifuatilia
hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya (hayupo
pichani) kwenye Mkutano Mkuu wa Wakandarasi hao uliofanyika jijini Dar es
Salaam leo Oktoba 12, 2023.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya akikabidhi tuzo kwa baadhi ya wadau waliowezesha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Wakandarasi wanawake uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 12, 2023.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...