SHIRIKA Lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO,) limeeleza namna linavyochochea Elimu ya Watu Wazima nchini kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC's,) ambavyo hutoa elimu kwa kundi hilo wakiwemo wanawake waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na hali duni ya maisha.
Akitoa mada katika Kongamano la maadhimisho ya Kitaifa ya Juma la Elimu kwa Watu Wazima kwa mwaka 2023 lililofanyika Kibaha, Pwani na kuwakutanisha wadau wa elimu wakiwemo maafisa elimu wa Elimu ya Watu Wazima, Mkurugenzi wa KTO Maggid Mjengwa amesema kuwa, kupitia program zinazotolewa katika vyuo vya maendeleo ya wananchi zimekuwa zikiwagusa watu wazima moja kwa moja na kuboresha maisha yao kupitia elimu ya darasani na elimu ya ziada ya ufundi, stadi za maisha na ujasiriamali na wamekuwa wakishirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kujibu changamoto mbalimbali za kijamii kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyopo kote nchini.
"Kwa kushirikiana na Wizara husika pamoja na wadau wa elimu na washirika wa maendeleo tumekuwa pamoja katika Kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kuyafikia malengo haya na hii ni pamoja na lile la kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda" ameeleza.
Amesema kuwa Programu ya Elimu haina mwisho inalenga kutoa maarifa na ujuzi kwa wanawake vijana na hiyo ni kwa kutoa mafunzo ya sekondari, elimu ya ufundi, ujasiriamali na stadi za maisha kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi;
"Vyuo hivi vilianzishwa mwaka 1975 kwa mawazo ya baba wa taifa na vimekuwa chachu ya maendeleo kwa kuwa vimekuwa vikitoa mafunzo nje ya mfumo rasmi kulingana na mahitaji ya wakati na eneo husika" amesema.
Aidha amesema kuwa vyuo hivyo vinatoa mafunzo kwa kila mwananchi bila kujali itikadi wala dini na kubwa zaidi na la kujivunia ni kuwa Tanzania ni nchi pekee barani Afrika yenye vyuo vya maendeleo ya wananchi ukitoa nchi za Sweden, Finland, Denmark na Norway ambazo hufanya idadi ya nchi tano duniani ambazo zina vyuo vya namna hiyo.
Amesema kuwa vyuo vya maendeleo ya wananchi 55 vilivyopo katika Mikoa yote nchini vimekuwa vikitoa huduma bora kwa washiriki hasa katika kuboresha mitaala na miundombinu ili kuwawezesha washiriki kunufaika na kutimiza ndoto zao.
Aidha ametoa mwito kwa watendaji hao kuwa mabalozi bora wa kuhamasisha jamii kutumia vyuo vya maendeleo ya wananchi kutumia fursa ya vyuo vya maendeleo ya wananchi kupata elimu katika mfumo usio rasmi pamoja na fursa za masomo ya ufundi, ujasiriamali na stadi za maisha bila malipo.
" Tukiwa tunaelekea Januari mwaka mpya wa masomo niwaombe tukawe mabalozi bora kwa jamii ili mabinti vijana waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito warejee shule kupita vyuo vya FDC's kote nchini na hata wale wa kiume kwa ada ya shilingi laki mbili na nusu kwa mwaka watapata fursa za kupata mafunzo ya ufundi... Serikali imewekeza kikubwa tushirikiane vijana wa kitanzania wanufaike." Amesema.
Licha ya kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia shirika la KTO pia Wana ushirikiano wa karibu na Shirikisho la mpira nchini (TFF) kupitia programu ya kukuza vipaji kwa vijana wanawake waliopo katika vyuo hivyo kupitia Program ya Mpira Fursa pamoja na program ya mafunzo ya ualimu wa chekechea yanayotolewa katika vyuo vya maendeleo ya wananchi vinavyopatikana kote nchini.
Baadhi ya mada mbalimbali zilizowasilishwa na kuunga mkono katika Kongamano hilo ni pamoja na kutolewa kwa Elimu ya Watu Wazima kwa kuzingatia usawa wa kijinsia pamoja na kutoa kipaumbele kwa makundi maalum, matumizi ya digitali katika kutoa elimu kwa walengwa hao, kuwepo kwa mkakati wa chakula shuleni kama ilivyo katika vyuo vya FDC'S pamoja na mikakati ya kukabili changamoto za rasilimali watu na Fedha zinazoikumba sekta hiyo katika utekelezaji wa majukumu.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO,) Maggid Mjengwa akifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali, Kulia ni Meneja Ugemaji Rasilimali Wilson Chacha kutoka mtandao wa Elimu Tanzania ( TEN-MET.)
Baadhi wa wananchi wakipata elimu kutoka Banda la KTO katika maonesho ya maadhimisho ya Kitaifa ya Juma la Elimu kwa Watu Wazima linalofanyika Kibaha Mkoani Pwani.
Kongamano likiendelea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...