Wataalam wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Oman wanakutana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili mashirikiano ya kuimarisha uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni kitaalam wa nchi hizo mbili.
Mkutano huo unaofanyika katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 6 - 7 Oktoba 2023 unajadili utekelezaji wa mashirikiano kwenye eneo la utafiti, maonesho, mifumo ya kidijitali na mafunzo ya utaalamu katika nyanja mbalimbali za uhifadhi wa Malikale
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii aliyewakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Dkt.Christowaja Ntandu amesema mashirikiano kati ya nchi mbili hizi ni ya kihistoria hivyo wizara inaunga mkono mashirikiano ya kuimarisha uhifadhi wa malikale.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Oman, Mhe. Jamaal Bin Hassan al Moosawi anayeongoza ujumbe wa watu saba kutoka katika Makumbusho ya Taifa ya Oman amesema jukumu lao kubwa ni kuhakikisha shughuli za uhifadhi na utafiti kuhusu urithi wa asili na utamaduni unafanyika kwa ubora na ufanisi.
Amesema kuwa uwepo wa kikao baina ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Oman utaongeza tija katika utekelezaji wa makubaliano baina ya nchi hizo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Lwoga amesema anaamini kutakuwa na matokeo chanya baada ya kikao hicho katika nyanja za uhifadhi, utafiti, kuingiza mifumo ya kidijitali kwenye mikusanyo na kuboresha miundombinu katika Makumbusho kupitia mashirikano na mafunzo mbalimbali yatakayowajengea uwezo wataalam wa Makumbusho zote mbili.
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...