Na Muhidin Amri,
Mbeya

MAKALI ya mgao wa maji  kwa wakazi wa jiji la Mbeya mkoani Mbeya, umepungua kutoka siku tatu kwa wiki hadi kufikia wastani wa saa 1 kwa siku,hivyo kutoa fursa kwa wakazi wa Jiji hilo kutumia muda wao kujikita katika shughuli za maendeleo badala ya  kwenda kutafuta maji.


Ni baada ya Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Jiji la Mbeya,kufanya ukarabati mkubwa wa chanzo cha maji cha Nzovwe-Iyela kwa gharama ya Sh.milioni 749,137,488.00 zilitolewa na Serikali kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19.


Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa Mamlaka hiyo Neema Stanton,  wakati akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea chanzo cha maji cha Nzovwe- Iyela.


Alisema,ukarabati wa chanzo hicho kumewezesha wananchi wa Jiji jilo kuwa na uhakika wa kupata huduma ya maji safi na salama,na ameishukuru serikali kutoa fedha ambazo zimesaidia mamlaka hiyo kuboresha huduma zake.


Stanton alitaja maeneo yaliyonufaika na fedha hizo ni Uyole,Forest mpya,Forest ya zamani,Mwanjelwa,Nzovwe,Simike,Veta na baadhi ya maeneo ya Soweto yenye takribani wakazi 55,000.


“ sisi kama mamlaka ya maji Mbeya tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita,imefanya jambo kubwa kwa sababu mradi huu umewezesha kupungua kwa kero ya huduma ya maji kwa maeneo niliyoyataja”alisema.


Alisema,katika maeneo hayo hali ya upatikanaji wa huduma ya maji imeboreka na hakuna tena mgao  na kuwataka wananchi kuhakikisha wanatunza chanzo hicho ili kiweze kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.


Diwani wa kata ya Iyela Mussa Ismail,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuboboresha sekta ya maji katika kata  ya Iyela kwa kutoa fedha ambazo zimemaliza kabisa changamoto  maji kwa wananchi.


Alisema,kabla ya chanzo hicho hali  ya huduma ya maji ilikuwa mbaya kwani wananchi walilazimika kuamka kati ya saa 10 na 11 alfajiri kwenda kutafuta maji kwenye maeneo yasiyo rasmi,hivyo kusababisha shughuli mbalimbali za maendeleo kusua sua.


Mkazi wa mtaa wa Airpot kata ya Iyela Agnes Njombe alisema,kupatatikana kwa mradi huo kumewezesha kupata nafasi ya kufanya shughuli zao  za maendeleo kwa kuwa hawapotezi muda wao tena kwenda mbali na makazi yao kwa ajili ya kufuata maji.


Agnes alisema,awali walikuwa wanatumia maji ya visima vya asili na wengine kununua maji kwa gharama kubwa,lakini sasa huduma  ya maji inapatikana kwenye makazi yao hali iliyohamasisha hata watu wengi kuingiza maji ya bomba ndani ya nyumba zao.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jiji la Mbeya Neema Stanton akionyesha chanzo cha maji cha Nzovwe-Iyela ambacho kimesaidia kuboresha huduma ya maji safi na salama katika Jiji hilo.
Baadhi ya miundombinu iliyojengwa kwenye chanzo kipya cha maji cha Nzovwe-Iyela ambacho kimewezesha kupungua kwa makali ya mgao wa maji kwa  baadhi ya mitaa ya Jiji la Mbeya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...