NA FARIDA MANGUBE MOROGORO
Shirika lake lisilo la kiserikali la Solidar Med, linalofanya kazi katika nchi tano duniani, wamekabidhi huduma ya kliniki inayotembea kwa Serikali ya wilaya ya Malinyi ili kuwawezesha wananchi walio kwenye mazingira magumu ya upatikanaji wa huduma ya afya kwa urahisi.
Meneja wa mradi huo Bi Frida Akyoo, akikabidhi rasmi kwa mkuu wa wilaya ya Malinyi Bw Sebastian Waryuba , kliniki hiyo ambayo ni gari maalum aina ya land cruiser lililoongezwa bodi maalum yenye hema, vifaa tiba na huduma zingine muhimu za kutolea huduma za afya, alisema linagharimu zaidi ya shilingi milioni 211.
"Wazo la kuleta kliniki hii lilitokana na kubaini baadhi ya wananchi wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, Baadhi wanatumia gharama kubwa kufika maeneo ya kutolea huduma za afya, Baadhi ya maeneo kutofikika kirahisi hasa wakati wa Masika"Alisema Meneja huyo.
Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Solidar med linalofanya kazi nchi za Tanzania , Lesotho,Msumbiji, Zambia na Zimbabwe, Dkt.Benatus Sambili,alisema shirika hilo lililosajiliwa kama NGO hapa nchini lililenga kuwafikia wananchi wa Morogoro hususani wanaoishi ukanda wa Bonde la Kilombero ikiwemo Ifakara,Mlimba, Ulanga na Malinyi.
Alisema Shirika hilo limekuwa likilenga kuboresha hospitali na utoaji wa huduma za afya, miradi ya mama na mtoto, afya ya Uzazi, huduma za mkoba za kifua kikuu na Ukimwi kwa kupeleka dawa na Tiba kwa walioandikishwa na sasa wameendelea kuongeza huduma zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Malinyi Bw Sebastian Waryuba, akipokea na kuzindua Rasmi kliniki hiyo katika viwanja vya hospitali ya wilaya ya Malinyi, aliwashukuru Solidar med na Serikali ya Uswiz kwa ujumla kutambua Kazi nzuri inayofanywa na Serikali hususani Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha huduma za afya na kuguswa kuunga mkono.
Kliniki hiyo inayotembea itakayokuwa na wahudumu wa afya, itatoa huduma zake kwa watu wote ikilenga zaidi huduma za mkoba kwa mama wajawazito na watoto wa umri wa chini ya Miaka mitano, magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwemo kisukari na shinikizo la damu, magonjwa ya kuambukiza ikiwemo kifua kikuu na virusi vya ukimwi, elimu ya afya ngazi ya jamii, vijana balehe na makundi mengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...