* Yaishukuru Serikali kwa jitihada za kutatua changamoto ya uhaba wa makazi, wafanyakazi...wananchi kunufaika na nyumba za kisasa

Na Leandra Gabriel, Michuzi Blog 

WAKALA Wa Majengo Tanzania (TBA,) imeendeleza kasi ya kupunguza changamoto ya uhaba wa makazi wa watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya majengo ya makazi kwa fedha za ruzuku kutoka Serikalini pamoja na fedha za ndani za Wakala hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua miradi ya nyumba za makazi kwa wafanyakazi wa Umma na wananchi kwa ujumla katika maeneo ya Temeke Kota, Magomeni Kota Phase II na Canadian Village Masaki jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Said Mndeme amesema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa muda mfupi wameonesha jitihada kubwa za kuhakikisha changamoto ya uhaba wa makazi inatatuliwa.

Amesema kuanzia Septemba 2021 mpaka sasa tayari Serikali tayari imetoa shilingi Bilioni 69.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo pekee fedha zilizoelekezwa katika miradi ya uendelezaji wa miliki kwa ujenzi wa majengo mapya ya Serikali na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Serikali.

Aidha ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kutoa miongozo na usimamizi wa Karibu wa Wakala hiyo katika kuyafikia mafanikio hayo kwa sasa.

Kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo katika Jiji la Dar es Salaam Mndeme amesema, miradi hiyo inakwenda vyema na TBA itaendeleza jitihada hizo katika kuhakikisha changamoto ya makazi inatatuliwa.

Amesema katika eneo la Temeke kota mradi wa jengo moja la sakafu tisa litakalobeba familia 144 umeanza na unatekelezwa na fedha za ruzuku kutoka Serikalini na mpango wa ujenzi katika eneo hilo ni majego Saba yenye uwezo wa kubeba familia 1008  na wamejipanga katika kukamilisha mpango wa ujenzi wa majengo yote saba katika eneo hilo.

Katika eneo la Magomeni Kota, Phase II amesema, utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za ruzuku kutoka Serikalini jengo moja limekamilika na limeanza kutumika na jengo la pili lipo katika hatua mwisho na umekamilika kwa asilimia 83 na kufikia Januari, 2024 litaanza kutumika.

"Tunashukuru Serikali kwa kuweka mkazo katika hili, tumepokea Fedha kwa ajili ya  kuanza ujenzi wa majengo mawili mapya hivi karibuni hapa Magomeni Kota, ili kufanikisha mpango wa kujenga majengo matano pale." Amesema.

Pia amesema, majengo 23 ya nyumba za makazi yatajengwa katika eneo la Canadian Village, Masaki na tayari ujenzi umeanza kwa fedha za ndani za Wakala hiyo na jengo moja lenye uwezo wa kubeba familia 12 limekamilika na majengo mawili yapo katika hatua za ujenzi na yamekamilika kwa asilimia 53 hadi kukamilika kwa majengo yote familia 472 zitaishi hapa." Amesema.

Mndeme amesema katika kuhakikisha kasi zaidi ya upatikanaji wa makazi Nchini Serikali imeridhia utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi na taasisi za kifedha na kabla ya mwisho wa mwaka watatangaza mradi huo wa Canadian Village kwa kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za kifedha kwa manufaa ya wananchi na wafanyakazi wa Umma.

Akizungumza kuhusu miradi hiyo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Dar es Salaam Arch. Bernad Mayemba amesema, miradi inayotekelezwa na wakala hiyo ni moja ya jitihada zinazofanywa na TBA katika kuhakikisha wafanyakazi wa Umma pamoja na wananchi kwa ujumla wanapata makazi bora yenye huduma muhimu.

Katika mradi wa Canadian Village unaotekelezwa na wakala hiyo kwa Fedha za ndani ameeleza kuwa; 

" Eneo hili lipo chini ya TBA mahususi kwa kutoa makazi ya wafanyakazi wa wananchi kwa ujumla....Eneo hili lina hekari 6.8 na tuna mpango wa kujenga makazi, eneo la biashara pamoja na vivutio mbalimbali." Amesema.

Amesema, Majengo mawili yanaendelea kujengwa kwa Fedha za ndani za wakala hiyo, na jengo moja lenye ghorofa tano lenye kubeba Kaya 12 na miradi hiyo miwili itatekelezwa kwa muda wa miwili na hadi kufikia Aprili mwaka ujao majengo haya yatakuwa yamekamilika tayari kwa kupokea wakazi.

Amesema kuwa katika utekelezaji huo wamepata kibali kwa kutekeleza miradi kwa watu binafsi ambao watajipatia makazi bora.

Aidha amesema kuwa eneo hilo la Canadian Village licha ya kujengwa majengo ya makazi pia yatajengwa  maduka makubwa ya biashara, maeneo ya kupumzika, maeneo ya kucheza watoto, gym na miradi yote hiyo imewekwa mifumo mahiri ya usalama ikiwemo lift, smart doors pamoja na mifumo ya uokozi (fire.)


Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Said Mndeme akizungumza mara baada ya ziara ya kukagua miradi ya majengo ya makazi yanayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kueleza kuwa TBA imejipanga katika kutatua changamoto ya uhaba wa makazi kwa kuhakikisha wanajenga makazi bora ya kisasa. Leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Mkoa wa Dar es Salaam Arch. Benard Mayemba akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara ya kukagua miradi ya majengo ya makazi yanayotekelezwa na Wakala hiyo jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa itakamilika kwa wakati na kwa viwango bora na mahitaji ya msingi. Leo jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa Majengo ya makazi yanayojengwa katika eneo la Canadian Village, Masaki jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Said Mndeme (kulia) akipata maelekezo ya utekelezaji wa mradi wa jengo la makazi Magomeni Kota, Phase II kutoka kwa Kaimu Meneja wa Wakala hiyo Mkoa wa Dar es Salaam Arch. Benard Mayemba kushoto,). Leo jijini Dar es Salaam.

Ziara ikiendelea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...