Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAMLAKA ya Usafiri w Anga Tanzania (TCAA) imesema tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa ndege, abiria, rada na mitambo ya kuongozea ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Dar es Salaam kuelezea sherehe za miaka 20 ya mamlaka hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Johari Hamza amesema kuwa usafiri wa anga umekuwa tegemeo kwa jamii hivyo lazima waendane na ukuaji wa soko hilo kulingana na idadi ya ndege zilizopo sokoni.
Hamza amesema mwaka 2003, idadi ya wakaguzi wa ndege waliokuwepo ni 28 na sasa wapo 44 hivyo, wanahitaji kuongeza idadi zaidi kwani ndege zinaendelea kununuliwa.
Pia lengo ni kuwdhibiti uchumi kwa kuhakikisha usafiri endelevu na unakuwa, mashirika kutoa huduma nzuri na abiria wafurahie huduma.
Amesema idadi ya marubani walikuwa 234 na mpaka sasa wapo 603, ndege zimeongezeka kutoka 101 hadi 206.
"Kwa miaka 20, idadi ya abiria imeongezeka kutoka 1,521,000 hadi abiria 5,723,000 ongezeko mwaka jana. Tumshukuru Rais Samia Suluhu kwa kazi kubwa aliyoifanya kupitia Royal Tour kwani idadi ya abiria na watalii imeongezeka, pia miruko ya ndege imeongezeka," amesema Hamza.
Kuhusu waongoza ndege kwenye minara yao walikuwa 70 sasa wamefikia 154 hivyo sekta inazidi kukua.
Pia amesema wahandisi wa mitambo ya kuongozea ndege wapo 44, wataalamu wa taarifa za kianga walikuwa 50 na sasa wapo 83 hivyo kwa kada nzima ya waongoza ndege wapo 281 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Amesema wana mpango wa kujenga majengo mapya kwa ajili ya chuo cha kisasa cha usafiri wa anga Afrika ili kudahili wanafunzi wa ndani na wa kimataifa.
Hamza ameeleza kuwa mamlaka hiyo ina rada nne za kuongozea ndege ambazo huangazia eneo lote la nchi kwa asilimia 100 ikilinganishwa na asilimia 25 ya wakati huo.
Amesisitiza pia, wana mitambo ya ardhini inayomsaidia rubani kutua na kupaa katika viwanja KIA, Zanzibar na Julius Nyerere na wanampango kufunga mitambo hiyo uwanja wa Mwanza.
"Serikali imetoa zaidi ya bilioni 35 mwaka Jana kwa ajili ya kuboresha mifumo ya sauti kati ya rubani na waongoza ndege na hivyo mawasiliano yataboreka na wateja wa kimataifa wataongezeka," amesema.
Pia amesema kuongezeka kwa ndege inaongeza fursa kwa wateja wao kusafiri kwenda maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi.
"Ushindani unapoongezeka kunatoa fursa kwa gharama za usafiri kuwa nafuu. Sekta hii iko vizuri kwa sasa na anga letu ni salama," amesema.
Ameongeza kuwa; "Tulnalenga kufumua mifumo ya zamani na kuweka mifumo mipya ya sauti Ili kuboresha mawasiliano kati ya rubani na waongoza ndege na kwamba mradi huo utakamilika Aprili 2024,"
Hamza ametaja changamoto zilizopo katika sekta hiyo kuwa no upungufu wa wataalamu katika sekta hiyo ambayo inakuwa kwa kasi hivyo, inabidi wawe na wataalamu wa kutosha.
Amesema watu wanaochukua masomo ya sayansi Bado wachache wanaupungufu wa marubani ambapo kwa ujumla walitakiwa wawe 783 upungufu uliopo ni takribani marubani 150 na wahandisi.
"Tumeanzisha mfuko wa marubani ambapo wadau wote wa anga huchangia ndio tunatumia fedha hizo kutangaza nafasi za wanafunzi mbalimbali waliosomea sayansi tuwasomeshe urubani nje ya nchi na gharama zake ni kubwa mpaka sasa marubani 28 tumewasomesha," amefafanua.
Amesema mkakati kusomesha wanafunzi chuo cha Taifa cha usafirishaji hivyo, itatusaidia kusomesha marubani wengi na tutafanya biashara hii vizuri.
Pia amesema miundombinu ya viwanja vya ndege baadhi vina changamoto kwani haviwezi kufikika wakati wa usiku au hata wakati mwingine.
Ameeleza ushindani katika sekta hiyo bado sio mkubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzisha kwa Mamlaka hiyo. aliyeko Kushoto ni
Daniel Malanga, Mkurugenzi Udhibiti Uchumi Kulia ni
Rashid Khamis Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usalama wa Usafiri wa Anga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...