Na Jane Edward, Arusha
Shule ya kiingereza ya Tanganyika School iliyopo jijini Arusha,inadaiwa kujihusisha na utoaji wa huduma ya Bima ya Afya kwa wanafunzi kinyume cha sheria bila kusajiliwa na mamlaka ya usimamizi wa Bima Nchini TIRA ambapo inadaiwa kukusanya takribani shilingi milioni 200 kuanzia mwaka 2014.
Hayo yamebainishwa jijini Arusha na Kamishna wa Bima nchini Dkt Baghayo Saqware ambapo amesema shule hiyo imekuwa ikiendesha huduma hiyo kwa kutoza ada ya Bima ya afya ya sh,200,000 laki mbili, kwa mwaka kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari na sh,90,000 kwa kila mwanafunzi wa Awali.
Amesema kutokana na kosa hilo la jinai chini ya kifungu cha 161(1)cha Sheria ya Bima sura namba 394 mtuhumiwa huyo anakabiliwa na adhabu ya kufungwa miaka miwili jela au faini ya shilingi milioni 5 .
" TIRA imejiridhisha kuwa shule hiyo inaendesha huduma ya Bima kwa kuwatoza wanafunzi ada ya Bima kinyume cha sheria na hivyo alimtaka mmiliki wa shule hiyo kulipa faini ya shilingi milioni 5 kwa mamlaka hiyo na kuacha mara moja kukusanya Bima ya Afya kwa wanafunzi hao kabla hatua kali kuchukuliwa dhidi yake"alisema
Kamishna ameielekeza shule hiyo kama inataka kutoa huduma ya Bima Kufanya utaratibu kusajili huduma hiyo kwa TIRA ikiwa kama bado anania ya kuendesha huduma hiyo .
Awali akizungumzia hatua za awali zilizo chukuliwa kabla ya kufikia kutoa taarifa kwa waandishi Dkt Saqware amesema mnamo januari 16 2023 ,TIRA ilipokea malalamiko kutoka kwa Alexander Lugale Oyuge mkazi wa Sakina jijini Arusha kuwa watoto wake wawili waliokuwa wakisoma katika shule hiyo,mmoja wapo alivunjika mguu lakini uongozi wa shule hiyo uligoma kumhudumia licha ya kupokea ada ya bima ya mzazi huyo.
Kamishna amesema kuwa mamlaka hiyo kupitia ofisi zake za kanda ya kaskazini ilifanyà ukaguzi katika shule hiyo na baadaye ilimwita kwa barua mmiliki wa shule hiyo aliyetambulika kwa jina la Brenda Mbori ambapo hakufika.
Michuzi blog haikuishia hapo ikautafuta uongozi wa shule hiyo na kuzungumza na Mhasibu ambaye alijulikana kwa jina moja la Eric ambapo ilisema madai hayo ni ya uongo na kukiri kweli waliitwa na TIRA lakini hawakuweza kufika kutokana na mkurugenzi wa shule hiyo kutokuwepo.
"Madai ya sisi kutoza wanafunzi pesa ya Bima hiyo siyo kweli na kweli tuliitwa ofisi za Tira mara mbili ambapo zote hatukuweza kufika kutokana na sababu mbalimbali lakini tuliandika barua ya kuelezea sababu ya kutofika na sio kukaidi kama Taarifa ya mamlaka hiyo inavyosema.Alisema
Hata hivyo Mamlaka ya Bima inaendelea kutoa onyo kali kwa Taasisi, Shule au mtu binafsi anayejihusisha na kutoa huduma za bima bila kusajiliwa kuwa atachukuliwa hatua kali za kisheria na kuwataka wazazi kujiridhisha na huduma za bima zinazotolewa na Mashule kabla ya kulipia.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...