Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WIZARA ya Maliasili na Utaliii imesema Serikali inatambua nafasi ya mchango wa vijana katika kushirikiana nao kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku ikisisitiza milango iko wazi kwa vijana wenye teknolojia bunifu ambazo zinalenga kukabiliana na athari hizo.
Aidha mikakati imeanzishwa kuwawezesha vijana kushiriki katika utunzaji wa mazingira na kumekuwepo na wiki ya ubunifu ambapo vijana wanashawishiwa kuonesha teknolojia bunifu ambazo zitatuondoa katika chnagamoto hizo za athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dustan Kitandula alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa Vijana Duniani kuhusu mabadiliko ya tabianchi mwaka 2023 ulioandaliwa na Kituo cha Uongozi wa Vijana wa Kimataifa kwa ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu ya Tanzania (TFS).
“Vijana ni taifa la leo na ndio taifa kesho na hapa wenyewe wameshaukubali ukweli huo.Ukiangalia takwimu zetu za sensa za watu na makazi zinatuonesha taifa hili ni la vijana kwani asilimia kubwa ya wananchi wa taifa hili ni vijana.
“Kwa hiyo lazima tuweke mkazo kuhakikisha ili kundi kubwa la vijana linakuwa na uelewa kwamba maisha ya leo na kesho yako katika mikono yao.Mikakati mbalimbali imeanzishwa kuwawezesha vijana kushiriki katika utunzaji wa mazingira.”
Amesisitiza kutokana na kutambua umuhimu wa kundi la vijana milango kwa Serikali iko wazi usaidizi uko tayari , hivyo wajitokeze wasaidiane nao katika kuweka mazingira katika hali salama.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kuja na mipango ya kupambana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi na kumekuwepo na mikakati ya kupandi miti katika nchi yetu kila mwaka.
“Inawezekana katika kupeana majukumu haya ya kupanda miti pengine hatujayasimamia vizuri kwamba wale tunaopewa jukumu la kupanda miti tukishapanda tunasahau kufuatilia kuhakikisha miti hiyo inaota na inakuwa.
“Kwa hiyo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametukumbusha tunapofanya mipango hii ya upandaji miti basi wanaopewa majukumu hayo wahakikishe miti hiyo inakuwa ili tuwe na uhakika jitihada hizo hazipotei. Kwa hiyo nitoe pongezi kwa jukwaa hili la mkutano wa dunia wa vijana ambao waliona ni vema wakaunga mkomo jitihada za serikali za kupanda miti katika maeneo yetu.
“Na wao walichagua eneo la ukanda wa bahari kwenda kupanda miti ya mikoko ambayo tunaambiwa yenyewe ndio inaweza kwa kiwango kikubwa kutusaidia kupambana na suala la hewa ya ukaa.Tunawapongeza TFS kushirikiana na vijana hawa kupanda miti ya mikoko,”amesema.
Ameongeza TFS imekuwa na mikakati ya kuhakikisha wanapanda miti ya mikoko katika fukwe zetu,kurejeshea uoto wa asili ambao umetoweka pamoja na kupanda miti kwenye baadhi ya maeneo yetu nchi nzima.
Ametoa rai kwa Watanzania kwamba jitihada hizo waziendeleze na pale ambapo wanakata mti basi wahakikishe wanapanda miti ili wote mwisho wa siku wawe salama kutokana na mambo hayo ya mabadiliko ya tabiachi.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo amesema waemekuwa na siku nne za kazi ambapo vijana wa Tanzania wameungana na vijana wenzao duniani kupaza sauti na kujengeana uwezo wa kuchukua uongozi katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
“Kwanza wamepata uzoefu na wameweza kukutana na manguli wanasayansi na watu wote wakubwa ambao wanajishughulisha na uhifadhi , mazingira na misitu kwa ujumla.Lengo kubwa lilikuwa kwanza kuwafanya vijana wajisikie wanawajibu wa moja kwa moja wa kuhifadhi mazingira na kuwekeza mawazo yao kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Na kazi kubwa ilikuwa kuwaonesha vijana katika kuhimili mabadiliko wanapaswa kufanya mambo ambayo hayapelekei tena kufanya mambo ya kuharibu mazingira , wawe na dhana ya kuuisha mazingira yetu yawe endelevu.Pia kupitia mkutano huu ilikuwa ni kufanya mambo katika ardhi moja kwa moja ambazo zinazosababisha kuongeza kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ndio waliamua kwenda kupanda miti ya mikoko katika fukwe za bahari.”
Aidha amesema katika maeneo mengi ya misitu vijana ndio wamebeba jukumu la ulinzi maeneo hayo wakishirikiana katika kupanga doria, kufanya kazi lakini kufanya shughuli mbalimbali za upandaji miti katika maeneo hayo iwe kwa kuajiriwa au kujitolea na huo ndio wajibu wao.
Profesa Silayo amesisitiza wataendelea kushirikiana na vijana wote wa Tanzania kupaza sauti na kuwaonesha ni wajibu wao kutekeleza jukumu hilo ili kuwa na kizazi ambacho kitakachokuwa salama na kwa kipindi kirefu wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa kuwashirikisha vijana kutumia nguvu zao sambamba na teknlojia kulinda mazingira.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...