Na Mwandishi wetu, Mirerani
MCHIMBAJI
wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara, Patrick Miroshi (Kipaa) amelalamika kwa Waziri wa Madini
Anthony Peter Mavunde kunyanganywa mgodi wake aliouchimba kwa zaidi ya
miaka 20.
Mgodi huo wa
madini ya Tanzanite unaolalamikiwa na Patrick Miroshi (Kipaa) upo kwenye
leseni namba PML 00416SMN ya Lema inayomilikiwa na kampuniya Njake
Enterprises.
Akizungumza
kwenye mkutano wa Waziri Mavunde na wadau wa madini ya Tanzanite mji
mdogo wa Mirerani, Kipaa amesema mdhamini wake waliokuwa wakifanya naye
kazi amemdhulumu mgodi wake.
“Kila
mtu hapa Mirerani anafahamu kuwa mgodi ule ni haki yangu na nimekuwa
masikini kwa kuuza mali zangu ikiwemo nyumba lakini mwisho wa siku
nikadhulumiwa akapewa tajiri,” amesema Kipaa.
Amesema
kuna mchezo mchafu ulifanyika kwa yeye kudhulumiwa mgodi wake kwa
sababu hana uwezo wa kifedha hivyo Waziri Mavunde amsaidie ili aweze
kupata haki yake.
“Huyu
mtu ambaye nilimkaribisha alikuja akapatiwa leseni yake karibu na mgodi
wangu na mwisho wa siku wakapima kwa kutumia GPS eti ikaonyesha mgodi
wangu upo eneo lake,” amesema Kipaa.
Hata
hivyo, Waziri Mavunde amemuagiza ofisa madini mkazi wa Mirerani (RMO)
Chacha Mwita kuingilia kati suala hilo kwa kupitia nyaraka zote na
kuhakikisha haki inapatikana.
“RMO
fuatilia hilo kwa kuita pande zote mbili zinazohusika juu ya
kuzungumzia umiliki wa mgodi huo wenye mgogoro kati ya watu hao wawili
tofauti,” amesema Waziri Mavunde.
Kwa
upande wake, RMO wa Mirerani Chacha ameahidi kushughulikia suala hilo
kwa kuziita pande zote mbili zinazolalamikiana na kupitia nyaraka zote
kisha kutoa uamuzi.
Hivi
karibuni, meneja wa mmiliki wa awali wa mgodi huo Mangoshi Seleman
ambaye aliuuza mgodi huo kwa Njake enterprises, Mohamed Mughanja amesema
mgodi huo ni halali kwa kampuni ya Njake.
“Sisi
tuliuuza mgodi huo kwa kampuni ya Njake enterprises jirani yetu akawa
analalamika kuwa amedhulumiwa mgodi jambo ambalo siyo kweli na Wizara
ilishatoa majibu kuwa mgodi ni wa Njake,” amesema Mughanja.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...