Mratibu Miradi ya CAMFED Mkoa wa Morogoro, Bi. Gloria Madafu akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha vijana 31 waliokatishwa masomo awali na baadaye kuwawezesha na kuendelea hadi kumalizia kidato cha nne.Mwanafunzi Ndewina Hawa aliyekatizwa masomo kwa ujauzito mkoani Morogoro akizungumza katika mkutano huo.Mwanafunzi Anna John aliyekatizwa masomo kwa ujauzito mkoani Iringa akizungumza katika mkutano huo.
Mwanafunzi Zainabu Shaban akizungumza na mwandishi wa habari hizi
Na Joachim Mushi, Dar


SHIRIKA la CAMFED Tanzania limewakutanisha baadhi ya wanafunzi waliokatishwa masomo yao, kabla ya kurejea na kuendelea na masomo tena baada ya agizo rasmi la Serikali iliyolitoa kuaruhusu wanafunzi hao maeneo mbalimbali nchini warudi Shuleni na kuendelea na masomo tena.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwenye mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mratibu Miradi ya CAMFED Mkoa wa Morogoro, Bi. Gloria Madafu alisema shirika hilo limewakutanisha vijana 31 waliokatishwa masomo awali na baadaye kuwawezesha kuendelea hadi kumalizia kidato cha nne.


Alisema CAMFED imewakutanisha wanafunzi hao ili kutathmini mradi wao uliolenga kuwarejesha wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, lengo likiwa ni kukutana na wasichana ambao CAMFED imeweza kuwasaidia kurejea shuleni, kwa kugharamia sehemu ya mahitaji ya msingi ili kufanikisha wao kurejea shuleni.


"...lengo la kuwakutanisha wanafunzi hawa ni kupata mrejesho kupitia kwao juu ya changamoto mbalimbali walizokutana nazo kipindi chote cha wao kurejea shule kwa ajili ya kuendelea na masomo yao waliyokatiza hapo awali. Changamoto hizi pamoja na mafanikio yatatuwezesha kujua nini cha kufanya ili kuongeza idadi ya wanafunzi kwa programu ya mwaka ujao," anasema Bi. Madafu.


"Siku ya leo tupo hapa na wanafunzi 31 kutoka mikoa ya Iringa, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro na Tanga, ambao walikatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, lakini baada ya tamko la Serikali kuruhusu kurejea tena shuleni Shirika la CAMFED likawawezesha mahitaji ya msingi na kufanikiwa kuendelea na masomo yao, kubwa ni kupata maoni na mrejesho kutoka kwao," alisema.


Alisema jumla ya wanafunzi 31 wamekutanishwa, huku kati yao watoto 11 walifanikiwa kurudi shuleni kupitia mfumo rasmi wa elimu na wengine 20 wemesaidiwa na mfumo wa elimu ya watu wazima kwa kushirikiana na Shirika la CAMFED Tanzania.


Alibainisha kuwa, kulingana na maandalizi na mikakati waliokwisha anza kuifanya ikiwemo kufanya mikutano na jamii, kukutana na viongozi mitaa, kata nayo kwa mwakani wamejipanga kuwezesha idadi kubwa ya wanafunzi wenye changamoto hizo.


Aliongeza kuwa, tangu mwongozo wa Serikali ulipotolewa tuliweza kukutana na viongozi wa vijiji, maofisa Elimu Kata na Jamii kwa ujumla ili kuhamasisha wanafunzi hao kurejea na kufanikiwa kuwarejesha shuleni wanafunzi 47.


Alisema baada ya kukutana na vijana hawa na kushirikishana changamoto na maoni yao, watarudi maeneo waliotoka na kutumika kama 'Champions' ili kuwashawishi na kuhamasisha vijana wengine ambao bado hawajarejea shuleni kurejea ili kuendelea kupambania kutimiza ndoto zao kielimu zilizokatizwa hapo awali.


"Kwa mwaka 2024 CAMFED Tanzania kupitia programu hii tunatarajia kuwarejesha takribani wanafunzi zaidi ya 200, hiki kikao ambacho tunakifanya leo tunatarajia wanafunzi hawa wataenda kutumika kama 'Champions' katika kuhamasisha wanafunzi wenzao waliokatisha masomo kwa njia mbalimbali kuweza kurudi shuleni, vijana hawa wapo ambao watatawanyika hata katika wilaya zingine na kutumika kutoa elimu ya uthubutu na ushawishi kwa wengine, kama mwongozo wa Serikali ulivyoonesha nmna ambapo kila mdau wa elimu anaweza kushiriki katika utekelezwaji wa utaratibu huo," alisisitiza.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wanufaika na programu hiyo wakizungumza kwenye mkutano, huo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa fursa alioitoa tena kwa wanafunzi waliokatizwa masomo yao kuweza kuendelea tena kutimiza ndoto zao kielimu.


Mwanafunzi Anna John aliyekatizwa masomo kwa ujauzito mkoani Iringa mwaka 2021 akiwa kidato cha kwanza anaishukuru Serikali kwa kutoa nafasi hiyo pamoja na Shirika la CAMFED Tanzania kwa kuwawezesha na hatimaye amerejea shuleni na kumalizia masomo yake.


"Binafsi sikupenda kujikuta naingia katika changamoto ya ujauzito uliokatiza masomo yangu, lakini baada ya baba yangu kufariki nilijikuta nakosa mahitaji ya msingi na kuangukia kwenye vishawishi vilivyosababisha nikapata ujauzito uliokatiza masomo yangu," alisema Mwanafunzi huyo.


Alishauri vijana wanaopata fursa ya kurejea shuleni kusoma kwa bidii ili kuweza kufikia ndoto zao kielimu, aliwataka kutokatishwa tamaa dhidi ya changamoto wanazokutana nazo wanaporejea kwenye masomo yao, bali wazitumie kama chachu ya mafanikio yao.


Naye Zainabu Shaban kutoka Wilaya ya Kilosa aliyekatizwa masomo mwaka 2021 kwa changamoto ya ujauzito akiwa kidato cha nne, anasema baada ya kupata taarifa Serikali imetoa fursa kwa wanafunzi hao kurejea alifanya hivyo kupitia msaada wa CAMFED na kufanikiwa.


"Naishukuru Serikali kwa kuturejesha shuleni, imetupa fursa nyingine ili tuweze kufikia malengo yetu kielimu,...nawashauri wasichana wenzangu waliopata changamoto kama yangu ya kukatizwa masomo waweze kurejea tena kupitia agizo la Serikali na kumalizia masomo yao kwani hii ni fursa nzuri ambayo tumepewa na mwanafunzi anaweza kumalizia masomo yake kwenye mfumo rasmi na usio rasmi ilimradi kufikia malengo yako," alisema.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...