Na Muhidin Amri,Tunduru

MRATIBU wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wilayani Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole,amewaonya waganga wa tiba asili na mbadala kuacha tabia ya kuwakumbatia wagonjwa wa kifua kikuu wanaofika kwenye vilinge vyao.

Badala yake,kuwapa rufaa ya kwenda Hospitali wakapate matibabu sahihi na kwa wakati ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na kifua kikuu.

Kihongole amesema hayo jana, wakati akizungumza na na wakazi wa kata ya Nanyoka katika kampeni inayoendelea ya uelimishaji,uchunguzi na upimaji wa ugonjwa wa TB kwa wananchi wa wilaya ya Tunduru.

Alisema,waganga wa tiba asili wanapaswa kufahamu na kuchangia mnyororo wa rufaa pale wagonjwa wanaofika kwenye vilinge vyao wanapobainika kuwa na ugonjwa unaohitaji matibabu ya Hospitali.

Mkansange ambaye pia ni mratibu wa tiba asili na mbadala wa wilaya hiyo alisema,wataanza msako na kuwakamata waganga wanaowakataza wananchi(wateja) wanaofika kwenye vilinge wakiwa na maambukizi ya kifua kikuu kuacha kutumia dawa za Hospitali.

“tiba za asili na mbadala zinakubali na zipo kisheria,lakini hatutaki waganga wazuie matumizi ya dawa za asili kwa wateja wanaofika kwenye vilinge vyao,hali hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo”alisema Kihongole.

Amewataka waganga wa tiba asili na mbadala,kushirikiana na serikali katika kuibua wagonjwa wa kifua kikuu wanaokwenda kwenye vilinge vyao huku wakiwa na maambuizi ya ugonjwa huo ili waweze kupatiwa matibabu badala ya kuwakumbatia.

Kwa mujibu wa Kihongole,kwenye vilinge vya waganga wa tiba asili kuna mkusanyiko wa watu wengi wenye shida mbalimbali wanaofika kwa ajili ya kupata tiba.

Alieleza kuwa,ni muhimu waganga kutambua kwanza matatizo ya mteja kabla ya kutoa tiba ili kufahamu kama anahitaji tiba ya asili au matibabu ya Hospitali ili kuepusha kuongezeka kwa magonjwa ya kuambukiza.

Baadhi ya wananchi,wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali waganga wanaowarubuni na kuwakataza wateja kutumia dawa za Hospitali kwani wamekuwa sehemu ya kuongezeka kwa madhara makubwa katika jamii.

Ali Yawani alisema,waganga wengi hawana utaalam wowote badala yake wanatumia maneno ya uongo kwa wateja wanaofika katika maeneo yao na wengine kupiga ramli chonganishi hali inayozalisha ugomvi kwenye familia na jamii.

Alisema,waganga wasizuiliwe kufanya shughuli zao,bali ufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini kama dawa zinazotolewa ni sahihi na zinaponya wananchi.

Haus Majua alisema, baadhi ya waganga wa tiba asili wamekuwa chanzo cha kuongezeka kwa ugonjwa wa kifua kikuu na ukimwi kwa kuwakataza wateja wao kutumia dawa za Hospitali.

Ameiomba serikali,kuwafuatilia ili kujua tiba zinazotolewa kama zina ukweli kwani baadhi yao ni waongo na wanatumia majani na mizizi ya miti kuwaongopea watu na kujipatia fedha.
Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole,akitoa elimu ya kifua kikuu kwa wakazi wa kata ya Nanyoka wilayani humo wakati wa kampeni ya uelimishaji,uchunguzi na upima wa vimelea vya Tb.

Baadhi ya wakazi wa Tunduru mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole wakati wa kampeni ya uelimishaji,uibuaji na uchunguzi wa vimelea kwa kifua kikuu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...