Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuwa Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mfano wa kuigwa kwa vijana wa Afrika, wakiwemo wa kike wanaotaka kuwa mahiri na kujenga ushawishi mkubwa katika maeneo mbalimbali ya uongozi kadri ya ndoto zao. 

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Anamringi Macha, Dusemba 12, 2023, alipokuwa akitoa salaam za CCM kuwakaribisha viongozi vijana wanawake kutoka nchi 16 barani Afrika, wanaoshiriki Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Young Women of Africa (YWOA), unaofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani. 

“Tunapozungumza muda huu kutoka hapa tulipo kuna idadi kubwa ya wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha ambao wamefanikiwa kubadilisha mtazamo na mwonekano wa jamii kuhusu wanawake, katika nchi zao, Afrika na dunia kwa ujumla, hasa kutoka kwenye mtazamo dhaifu na kuwa mtazamo wa uimara na umakini.”

“Wamekuwa mfano wa kuigwa kwa namna ambavyo wameweza kudhihirisha pasipo shaka yoyote kuhusu uwezo na nguvu za mwanamke.”

“Kwenye nyanja ya siasa, hapa tunaye Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, ambaye umahiri, uimara na uwezo katika uongozi, unatambuliwa na kukubalika duniani kote sasa. Wiki iliyopita tu, Jarida la Forbes limemtaja kuwa ni mmoja wa wanawake 100 wenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani,” amesema Ndugu Macha. 

Akiwasisitiza kuhusu umuhimu wa kujiamini kwa kutumia dhana ya uwezo wa mwanamke, kuliko kujikita kwenye udhaifu zaidi, Ndugu Macha pia aliwapatia mfano wa Mgombea Urais wa Chama cha SWAPO cha Namibia kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwaka kesho, akiwaambia kuwa ni mfano mwingine wa jinsi ambavyo wanawake wanapaswa kubadili mitazamo ya dhana dhalili. 

“Tunapozungumza hapa, wenzetu SWAPO wa Namibia, wanajiandaa na uchaguzi na mgombea wao wa Urais ni mwanamke…kwa hiyo nao wanajiandaa kutufuata sisi Tanzania kwa kuwa na Rais mwanamama. Mifano hii tunayo kwenye nyanja zote za maisha sasa, hata zile zinazoendesha dunia, iwe kwenye kisiasa, iwe taaluma, michezo na zingine zote utakazoweza kusema. Kwenye chumba hiki tuna mfano wa Profesa Marcellina Chijoriga. Mnaona jinsi anavyosimamia na kuendesha shule hii kwa viwango na muonekano wa kimataifa,” amesema Ndugu Macha. 

Alitoa wito kwa viongozi vijana wanawake kutokuwa wanyonge katika kuhakikisha wanatimiza ndoto za mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali katika maisha yao. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...