Tanzania imeng'ara katika tuzo za kimataifa za Utalii zilizotolewa na World Travel Awards (WTA) wakati wa sherehe za kutimiza miaka 30 ya tuzo hizo zilizofanyika katika mji wa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, Disemba 2, 2023
Katika tuzo hizo, Kisiwa cha Thanda kilichopo katika eneo tengefu la Shungimbili, Wilayani Mafia, Mkoani Pwani kilitangazwa kuwa kisiwa bora cha kipekee duniani (World Leading Exclusive Private Island).
Kisiwa hicho kinachosimamiwa na Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambacho ndani yake kuna hoteli yenye hadhi ya nyota tano kimeshinda tuzo hiyo kwa mara ya Saba mfululizo.
Halikadhalika, Kisiwa hicho pia kilitangazwa kuwa Kisiwa Bora cha Kipekee barani Afrika kwa mwaka 2023.
Mbali na tuzo hiyo ya Thanda Island, Tanzania ilipata tuzo ya nchi inayoongoza duniani katika utalii wa mbugani (World Leading Safari Destination) kwa mwaka 2023 ambayo ilipokelewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Uleg kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii.
Tuzo hizo zilitolewa kando ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP 28) unaoendelea katika mji wa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo Mhe. Ulega anahudhuria.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...