Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimeanza kutoa mafunzo kwa wahudumu wa kwenye mabasi ya abiria ili kuifanya kazi hiyo kuheshimika kama zilivyo fani zingine.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga wakati wa uzinduzi wa kozi hiyo na kuongeza kuwa, katika kuunga mkono juhudi za serikali CBE imeamua kutoa mchango wake katika kukuza weledi na ufanisi wa wahudumu wa usafiri wa umma.

Amesema lengo ni kuhakikisha huduma hizo zinakuwa na ubora wa hali ya juu na kwamba CBE ni miongoni mwa taasisi ambazo zimepewa kibali cha kutoa mafunzo hayo.

"Chuo tayari kimeshaandaa mitaala, mwongozo wa mafunzo, pamoja na kuandaa wawezeshaji na vitendea kazi vyote muhimu kwa mafunzo hayo yatakayochukua siku kumi, hivyo matarajiio yetu kuwa mara tu baada ya uzinduzi huu chuo kitaanza rasmi udahili wa washiriki wa mafunzo na yatafanyika katika vituo vilivyoko katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya. Amesema Prof. Lwoga.

Amesema CBE inatambua juhudi zilizofanywa na serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), katika kuboresha usafiri wa barabara nchini.

Alisema kuanzishwa kwa LATRA kupitia Sheria ya Udhibiti wa Usafiri ya mwaka 2019 ilikuwa hatua muhimu katika kusimamia na kuboresha sekta hiyo muhimu.

“Hata hivyo bado tunashuhudia sekta hii ikiendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uvunjifu wa sheria na kanuni za usalama barabarani, huduma kwa wateja isiyoridhisha hali hii inahitaji jitihada zaidi kutoka kwa wadau wote.” Amesema

Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi, Michaek Deleli, amesema Jeshi hilo linaona mafunzo hayo ni fursa kubwa kwasababu yataondoa changamoto nyingi za barabarani kwenye usafiri wa umma.

“Kuna mambo yanafanyika ya kiuhalifu kwenye usafiri wa umma na yanatokana na wahudumu kutokuwa na elimu sahihi, mfano tumeshuhudia kusafirishwa kwa wahamiaji haramu vitendo vinavyofanywa na wahudumu wasio na mafunzo wala kujua sheria za nchi.” Amesema

Amesema hata dawa za kulevya zinasafirishwa kupitia magari hasa mabasi lakini yanapokamatwa wahudumu wanashindwa kuwatambua wamiliki hali ambayo imekuwa ikisababisha chagamoto.

“Kwa mfano tunapokamata mzigo haramu kwenye basi unakuta mhudumu wa basi hajui ni wa nani na ukiwauliza hata abiria wanaukataa lakini wakipata mafunzo haya wataweza kuweka mizigo kwa namna ambayo kila mwenye mzigo atatambulika kwa urahisi.” Ameongeza.

Naye mweka hazina wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mbazi Mjema ameipongeza serikali kwa uamuzi wa kuanzisha mafunzo hayo kwani yatasaidia chama hicho kutimiza majukumu yake na utendaji wa kazi utaboreshwa.

“Tunawafanyakazi wengi wa darasa la saba kwa hiyo vyeti watakavyopata ni mali yao wakihama kampuni moja kwenda nyingine cheti kinabaki ni mali yake binafsi kwa hiyo tupunguzieni ada ya mafunzo ili tuweze kuwapeleka mafunzo wahudumu wengi.” amesema

 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo katikati akitaka utepe kuzindua mitaala itakayotumiwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kufundisha wahudumu wa kwenye mabasi mara baada ya uzinduzi wa kozi hiyo chuoni hapo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi, Michaek  Deleli, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara (LATRA), Johansen Kahatano na wapili kutoka kulia ni Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...