Na Eleuteri Mangi, WANMM


Tanzania itekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ambao chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kupanga, kupima, kumilikisha na kutoa hati miliki za ardhi kuongeza usalama wa milki za ardhi nchini.


Akihitimisha Kikao Kazi cha Asasi za Kiraia ambacho kimefanyika kwa siku mbili hivi karibuni jijini Dodoma, Mratibu Msaidizi wa Mradi huo Dkt. Upendo Matotola amesema mradi huo unatumika kama mfano kwa ulimwengu na kuwasisitiza washiriki hao kuijenga nchi kwa pamoja ili kujenga taswira njema ya Tanzania kimataifa.


“Tunajua kabisa tunapopanga, tunapopima, na kumilikisha vipande vya ardhi, Uchumi wetu unaongezeka kwa sababu ardhi iliyopangwa na kupimwa inaongezeka thamani na inapoongezeka thamani, shughuli za kiuchumi nazo zinaongezeka” amesema Dkt. Upendo.


Katika kutekeleza mradi huo, Dkt. Upendo amesema kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kijamii katika kutekeleza masuala ya ardhi na kusisitiza kuwa Serikali itabaki na jukumu la kujenga uwezo, mazingira wezeshi, utawala na usimamizi wa ardhi nchini.


Akizungumza na washiriki hao Dkt. Upendo amesema, “Sisi wote ni wazalendo, tunapenda mradi huu uendelee kutekelezwa vizuri kama ulivyokusudiwa kuleta matokeo chanya yenye tija kwa taifa letu ili kutoa fursa kwa miradi mingine kutekelezwa hapa nchini, tunaposema vibaya kuhusiana na mradi, tunajichafua wenyewe.”


Aidha, amewasistiza washiriki hao kuwa ufanisi wa mradi huo unategemea ushiriki wao mzuri kwa kutoa utaalamu wao kwa kufanyakazi kwa uaminifu na uadilifu kwa uzalendo kwa kutanguliza maslahi ya taifa lao.


Kwa upande wao mshiriki wa kikao kazi hicho Bw. Innocent Jaji kutoka Maswa na Bi. Mariam Mohamed kutoka Mvomero wamesema kuwa Asasi za Kiraia zinajukumu la kushirikiana na serikali katika kutelekeza mradi huo kwa kutoa elimu ya masuala ya ardhi makundi maalumu wakiwemo wanawake, wazee, watoto na watu wenye ulemavu wapate haki zao katika umiliki wa ardhi.


Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ambao unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia umeanza kutekelezwa mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika 2027 ambapo jukumu lake ni kurasimisha ardhi kwa wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...