SERIKALI imeipongeza Kampuni ya Bima ya First United Takaful kwa kuanzisha huduma za kibima zitakazoweza kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa ujumla pamoja na sekta ya fedha ya mwaka 2020 mpaka 2030 inayotoa dira kwa sekta ndogo ya bima sambamba na maelekezo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar.
Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Uchumi wa Zanzibar, Dk. Saada Mkuya wakati akizindua kampuni hiyo pamoja na huduma ya bima ya Takaful inayofuata misingi ya dini ya kiislamu jijini Dar es Salaam jana akisema uzinduzi huo unaunga mkono juhudi za Rais wa jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya bima.

“Moja ya malengo ya kimkakati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ni kuhakikisha tunakuwa na bidhaa mpya 10 hadi kufikia mwaka 2030, baadhi ya malengo ikiwa ni kuakikisha asilimia 90 ya watu wanapata bima ya afya ikiwa ni pamoja na kuwa na nia nane za kusambaza bima kwa bei nafuu. “Tuna pengo kubwa la watu kutokufahamu, nini maana ya bima, kutofikiwa ama kutojua nini faida ya bima, First United Takaful, mbali na malengo yenu, nataka muwe tunu ya kufikisha ujumbe kwa wananchi walio wengi kuona kuna umuhimu wa kuwa na bima hususan Takafula”, alisema Waziri Saada.

Aidha alisema Serikali zote mbili zimedhamiria kuendelea kuweka mazingira tulivu kwa ajili ya uwekezaji wa Takaful ambao una tija hivyo maendeleo na mageuzi katika sekta ya bima kutimia endapo sekta hiyo itapita katika ubunifu na matumizi ya kiteknolojia.

“Tunaishukuru TIRA kwa kuchukua hatua hii ya kuruhusu huduma za bima inayofuata misingi ya kiislamu, ambayo ni muhimu kwa wateja wote waislamu na wasio waislamu, tuwashukuru sana sababu mmeshaweka msingi mzuri”, aliongeza mheshimiwa Waziri Saada.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Kamishna wa Bima, Bi. Khadija Issa Said aliipongeza kampuni ya First United Takaful kwa kuwa kampuni ya pili nchini kwa kupata leseni ya kutoa huduma za bima zinzzofuata misingi ya kiislamu ya Takaful.

“Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini itafanya kazi kwa karibu na wadau wote wa bima na kuweka mazngira wezesha katika soko la bima hususan Takaful ili huduma hizo ziweze kuleta tija kwa wananchi”, alisema Bi. Khadija.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa First United Bwana Abdulnassir Ahmed Mohamed alisema bima imekuwa ni kiunganishi muhimu sana kwenye maisha ya kila siku, kisheria, kijamii na kiuchumi kwani ukiwa na bima inakupa utulivu wa nafsi na ulinzi binafsi na mali katika vipindi mbalimbali vya changamoto.

“Pamoja na hayo yote, bado pamekuwepo na changamoto kwenye upatikanaji wa huduma ya bima inayokidhi mahitaji ya Imani zao za kiroho, hivyo bima ya Takaful yenye mazingatio ya Sharia za Imani ya kiislam, ambayo msingi wake ni kanuni za ushirikiano, uchangiaji wa majukumu kwa pamoja, ulinzi wa pamoja kwa washiriki, wachangiaji, na ushirika wa manufaa kwa pamoja pale ambavyo mmoja wa wachangiaji hupata changamoto bila ya kutegemea itaenda kuwa mkombozi kwa wale wenye uhitaji wa bima hiyo.

“Zipo aina mbalimbali za bima ya Takaful tunazotoa kama vile bima ya maisha, mali, na bima ya kawaida, na kuhakikisha kuwa wateja wetu wanapata bima kamili kulingana na mahitaji yao maalum, tukiwekeza katika rasilimali muhimu ya wafanyakazi wataalamu katika kukuza maeneo ya ubunifu na yenye kuzingatia wateja”, alisema Bwana Mohamed.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni hiyo, Dk. Kassim Hussein alisema wakiwa kama waanzilishi katika tasnia hiyo kwa Tanzania Bara katika kutoa bidhaa mbalimbali za Takaful zinazowapa usalama na amani Waislamu na wasio waislamu, wakijikita zaidi katika kuleta masuluhisho katika kanuni za ushirikiano na msaada wa pande zote kwa uwazi, usawa, na kuepuka mambo ambayo yanapingana na imani za Kiislamu.

“Ni muhimu kutambua kuwa Takaful sio tu bidhaa, inawakilisha mabadiliko makubwa katika tasnia ya bima, ni uthibitisho wa azma yetu ya kuhudumia wateja wetu mbalimbali kwa uaminifu na uelewano, tunasadiki kwa dhati kuwa bima inapaswa kuwa inapatikana kwa wote, bila kujali imani zao za kidini, na Takaful inatuwezesha kufikia hili bila kuhatarisha maadili ya kiadili.

“Tunapoanza sura hii mpya ya Takaful, tunatambua jukumu kubwa lililo mbele yetu, tunaelewa kuwa lazima tuwe na ubunifu wa mara kwa mara, kubadilika, na kukabiliana na changamoto zitazotukabili, tuwahakikishie kuwa, tutaendelea kujitoa na kubaki kwenye viwango vya juu vya weledi, wajibu wa fidia, na kuridhika kwa wateja”, aliongeza Dk. Hussein.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...