Na Mwandishi wetu, Nyasa

WAKALA wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,kwa mwaka wa fedha 2023/2024,umepokea Sh.bilioni 2.434 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara wilayani humo.

Meneja wa Tarura wilaya ya Nyasa Mhandisi Thomas Kitusi alisema,kati ya fedha hizo Sh. milioni 934 zinatoka mfuko wa barabara,Sh.milioni 500 za mfuko wa Jimbo na Sh.bilioni 1 fedha za tozo na zitatumika kujenga barabara za lami za mitaa na barabara katika mji wa Mbambabay.

Alisema,kama wilaya wamekubaliana kila mwaka kuhakikisha wanajenga angalau barabara ya kilomita 1 ya lami katika mji wa Mbambabay na walianza mpango huo tangu mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo walijenga barabara moja ya na kufunga taa.

Alisema,ujenzi wa barabara za lami katika mji wa Mbambabay unalenga kuboresha mji huo maarufu kwa shughuli za utalii ili kuvutia shughuli za utalii na uwekezaji.

Kitusi,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuiongezea fedha Tarura kwa ajili ya ujenzi na kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo ambazo zimewezesha kuimarika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya na mkoa wa Ruvuma wenye utajiri mkubwa wa rasilimali ikiwemo ziwa nyasa.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Mbambabay wameipongeza serikali ya awamu ya sita kuanza ujenzi wa barabara za lami za mitaa zinazokwenda kuhamasisha na kuchochea shughuli za kiuchumi hasa utalii katika wilaya hiyo.

Joackim Kamanga(Bulushi)alisema,mji wa Mbambabay kwa muda mrefu barabara zake zilikuwa za vumbi,hivyo kusababisha uendelezaji wa mji huo kwenda kwa kusua sua,hivyo ujenzi wa barabara za lami za mitaa utaufanya mji huo kukua kwa haraka na kuvutia wageni hususani watalii wa ndani na nje ya nchi.

Kamanga,ameiomba serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)kuendelea kujenga barabara nyingi za lami ili mji huo uendane na umaarufu wake kwa kuwa kuna vivutio vingi.

Aidha,amewaomba wananchi wenzake wa Mbambabay kuanza kubadilika kwa kujenga nyumba za kisasa ambazo zitakuwa sehemu ya kuhamasisha watu mbalimbali kwenda kuwekeza na kuishi katika mji huo na maeneo mengine ya wilaya ya Nyasa.

Sholastika Challe alisema, hatua ya serikali kujenga barabara za lami katika mji wa Mbambabay zimeanza kushawishi watu kutoka nje ya wilaya ya Nyasa kuwekeza miradi ambayo imesaidia hata wananchi hasa vijana kupata ajira za muda za kudumu.

Anyitile Mwangosi mfanyabishara wa viywaji,ameishukuru serikali kwa kuboresha huduma muhimu za kijamii na mazingira ya mji wa Mbambabay wenye umaarufu mkubwa hapa nchini.

Hata hivyo,ameiomba kuendelea kuimarisha baadhi ya huduma ili wananchi waweze kuzitumia katika shughuli zao za kujipatia kipato ambazo zitasaidia kuongeza pato la Taifa.
MWISHOO.

 

Baadhi ya barabara za lami zilizojengwa na wakala wa barabara za mijini na vijijini(TARURA) katika mji wa kitalii wa Mbambabay wilayani humo kama zinavyoonekana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...