* TATOA yashauri elimu ya bima kuendelea kutolewa zaidi
* NIC yajipanga kulipa fidia ndani ya saa 24

CHAMA Cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA,) kwa kushirikiana na Shirika la Bima la Taifa (NIC,) wamefanikisha mchakato wa kulipa fidia kwa wahanga wa malori yaliyokuwa na kinga ya bima 22 ambayo yaliteketea kwa moto Nchini Congo mwaka 2014.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa TATOA Elias Lukumay amesema, kwa miaka nane tangu kutoka kwa ajali hiyo TATOA kwa kushirikiana na Shirika la Bima la Taifa (NIC,) wamekuwa wakifuatilia malipo hayo kutokana na hasara iliyotokea huku walengwa wakiwa waliopoteza magari ambayo yalikuwa na bima.

"Hadi kukamilika kwa mchakato huu fedha za chama ambazo hazitarejeshwa zimetumika katika ufuatiliaji nchini Congo.... Tunashukuru Serikali kupitia NIC kwa ushirikiano hadi kufanikisha mchakato huu uliodumu kwa miaka nane." Amesema.

Aidha amewataka wanachama wa TATOA kufanya kazi na kampuni za bima zinazotambulika ambazo pia zinatakiwa kuipa jicho changamoto ya mlolongo mrefu wa ulipaji fidia pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwa na kinga ya bima.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC,) Karimu Meshack amesema kuwa, shirika hilo ndio wasimamizi wa Soko la pamoja la Mashariki na Kusini mwa Africa (COMESA,) nchini na wahanga wa ajali hiyo iliyotokea nchini Congo ni wateja wao.

"Taratibu za COMESA likitokea jambo taratibu hufanywa na nchi ambayo tatizo lilitokea hii ikawa ni kikwazo katika kufanikisha jambo hili kwa wakati kutokana na ufinyu wa ushirikiano hali iliyopelekea nchini wanachama kuingilia kati." Amesema.

Meshack, amewataka wahanga pamoja na wanachama wa TATOA kutunza nyaraka wanazifanyia kazi ikiwemo kadi ya gari na leseni za madereva ili kutokwamishwa mchakato pindi majanga ya namna hiyo yanapotokea na kueleza kuwa kila mhanga atapata anachostahili.

Kuhusiana na utaratibu malipo ya fidia kwa wahanga pindi yanapotokea majanga, Meshack amesema, NIC hulipa madai ndani ya siku saba pekee na kuna mpango wa kufanya malipo ndani ya saa 24 kulingana na utaratibu wa madai.

Pia amewataka watanzania na nchi jirani kufanya kazi na shirika hilo ambalo limekidhi vigezo vya Kimataifa ili kujiweka salama zaidi pindi yanapotokea majanga ya namna hiyo.

Eva Joseph mmoja ya wahanga waliopoteza mali zao katika janga hilo ameishukuru TATOA kwa jitihada za kufanikisha ulipwaji wa fidia na kuwashauri wamiliki wa malori kukata bima katika ofisi zinazotambulika ili kujiwekea salama zaidi.

"Wasafirishaji tufanye kazi kwa kufuata sheria na utaratibu ulionyooka hususani kuwa na bima katika ofisi zinazotambulika... Tunashukuru Serikali kupitia NIC pamoja na TATOA kwa ushirikiano na uwazi katika ufuatiliaji." Amesema.

Vilevile ameshauri kuendelea kutolewa kwa elimu ya bima itakayowasaidia wafanyabiashara hao kufanya chaguzi sahihi zitakazowaweka salama pindi majanga mbalimbali yanapotokea.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA,) Elias Lukumay akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kukamilika kwa mchakato wa fidia kwa wahanga waliopoteza magari katika ajali ya moto nchini Congo na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano walioonesha. Leo jijini Dar es Salaam.

Mmoja ya wahanga waliopoteza malori katika ajali hiyo Eva Joseph (kushoto,) akizungumza wakati wa mkutano huo na kuishukuru TATOA kwa kuonesha ushirikiano pamoja na uwazi wakati wote wa mchakato wa ufuatiliaji. Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC,) Karimu Meshack (kushoto,) akizungumza kuhusiana na mchango wa Shirika hilo katika kufanikisha zoezi hilo na kueleza kuwa NIC wamejipanga katika kufanya malipo ndani ya saa 24 kulingana na utaratibu wa madai. Leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...