WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kufika katika ofisi za wakala wa Maji na usafi Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Lindi (LUWASA) kufuatilia mapungufu yaliyopo ikiwemo kutotumika kwa gari la uchimbaji visima lililotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu Juni, 2023 ili kuwezesha uchimbaji wa visima vya maji.
 
“Hii wizara ina Waziri makini sana, mnafanya vitu kwa ufichouficho, sasa Waziri aje hapa, mnamuona anavyohangaika Waziri wenu, vitu vidogo vidogo hivi mpaka waziri aje na ninyi mpo, kwanini mpo hapa,” Waziri Mkuu alisisitiza na kuongeza kuwa anahitaji taarifa ya kwa nini mashine hiyo tangu imefika haijachimba kisima hata kimoja.
 
Ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Januari 8, 2024, baada ya kufanya ziara katika ofisi za RUWASA zilizopo Manispaa ya Lindi na kushuhudia mtambo wa kuchimba visima ukiwa umeegeshwa na hakuna kisima kilichochimbwa tangu ulipotolewa mwaka jana huku katika mikoa mingine iliyopewa mtambo kama huo visima vinachimbwa kama ilivyokusudiwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alihoji sababu ya kutotumika kwa pikipiki zilizonunuliwa na RUWASA Mkoa wa Lindi tangu mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa jumuiya za watumia maji kwa madai kuwa bado hazijapata usajili. “Huu ni uzembe haiwezekani fedha za wananchi zinapotea nyie mpo tu. Hizi pikipiki zimeanza kuharibika.”
 
Akizungumzia kuhusu pikipiki hizo Afisa Manunuzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) Bw. Kenedy Mbagwa alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia suala la vibali vya kutumia pikipiki hizo kutoka makao Makuu ya RUWASA bila ya mafanikio, ambapo Waziri Mkuu baada ya kupata maelezo hayo amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Lindi afuatilie suala hilo.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua pikipiki zilizotelekezwa kwenye stoo ya Wakala wa Maji na usafi na Mazingira Vijijini, (RUWASA) Mkoa wa Lindi, alipofanya ziara katika ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo Manispaa ya Lindi Januari 8, 2024. Pikipiki hizo zilinunuliwa mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa Jumuiya za Watumiaji maji Mkoa wa Lindi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua moja ya mtambo uliotolewa na Serikali kwa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini, (RUWASA) kwa ajili ya kuchimba visima Mkoani humo, alipofanya ziara katika ofisi za Mamlaka hiyo Januari 8, 2024. Tangu kupokelewa kwa mitambo hiyo mwezi wa sita mwaka jana mitambo hiyo haijafanya kazi iliyotarajiwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...