Na Mwandishi wetu, Nyasa

WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Nyasa,uko hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji Ngumbo utakaohudumia wakazi 11,080 wa vijiji sita katika kata ya Ngumbo kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 4.6.


Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila,amevitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Hinga,Mbuli,Ngumbo,Mkili,Yola na Liwundi.


Kwa mujibu wa Samila,mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza umetekelezwa katika kijiji cha Hinga ambacho wananchi wameanza kupata huduma ya maji safi na salama na fedha zilizotumika ni Sh.bilioni 2.6.


Masoud amezitaja kazi zilizofanyika katika awamu hiyo ni kujenga matenki mawili moja la lita 75,000 na lingine lita 200,000,kujenga chanzo,(Intake),vituo vya kuchotea maji na kulaza bomba za kusambaza maji umbali wa kilomita 23.


Alisema,awamu ya pili inahusisha kazi ya kulaza bomba za kusambaza maji umbali wa kilomita 29.5 na kujenga vituo vya kuchotea maji 30 katika vijiji vitano vilivyobaki kazi itakayogharimu Sh.bilioni 2,030,668,500.

Ametaja kazi zinazofanyika ni kulaza bomba za kusambaza maji urefu wa kilomita 29.5 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 30 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 25 na utakamilika ifikapo mwezi April mwaka huu.


Katika hatua nyingine Samila alisema, wilaya ya Nyasa ina jumla ya vijiji 84 kati ya hivyo vijiji 46 vinapata huduma ya maji ya bomba na vijiji 38 vilivyobaki vinapata huduma ya maji kupitia visima vya asili na vyanzo mbalimbali.


Alisema,katika bajeti ya mwaka 2023/2024 Ruwasa wilaya ya Nyasa ilipanga kukamilisha miradi 6 ambayo ilipangwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na miradi mipya 3.

Aidha alisema,kabla ya Ruwasa haijaanzishwa mwaka 2019 upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya hiyo ilikuwa asilimia 39,lakini hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2023 huduma ya maji ni asilimia 53.


Ameishukuru serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ambayo itakapokamilika, itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 53 hadi kufikia asilimia 85 kwa upande wa vijijini na asilimia 95 meneo ya mjini.


Mkazi wa kijiji cha Hinga Rehema Ndomba alisema,kabla ya kujengwa kwa mradi huo walikuwa wanatumia maji ya ziwa nyasa na maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa safi na salama hasa wakati wa masika.


Nives Chiwangu,amewapongeza wataalam kutoka wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya na mkoa wa Ruvuma kwa kusimamia vizuri na kukamilisha kwa wakati, na hivyo kuwaondolea adha kubwa ya upatikanaji wa huduma yam aji katika kijiji hicho.


Mwenyekiti wa kijiji hicho Filbert Mapunda,amempongeza na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea mateso wanawake wa kijiji hicho ambao awali walitembea umbali mrefu hadi ziwa nyasa kwa ajili ya kwenda kuchota maji.
 

Msimamizi wa mradi wa maji  Liuli unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) Petro Mbele aliyeinama kushoto, akiwaonyesha wajumbe wa kamati ya  ujenzi wa mradi wa maji waliosimama kulia,  koki  inayotumika kutoa  maji kwenda kwenye makazi ya wananchi,wa pili kushoto meneja wa Ruwasa wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila na wa tatu kutoka kushoto kaimu Afisa Habari wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo.
 

 Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila kushoto,akisimamia zoezi la kuchota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji(DPS) kwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha Hinga wilayani humo jana.
 

Diwani wa kata ya Ngumbo katika Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma Kosmas Nyoni,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Hinga  Nives Chiwangu jana,baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi wa maji Ngumbo  ambao utakwenda kuwanufaisha zaidi ya wakazi 11,080 wa kata ya Ngumbo na Liwundi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...