Benki ya Exim imetangaza ripoti yake ya kifedha ya Mwaka 2023, inayoonesha mafanikio makubwa katika njanja mbalimbali ikiwemo ongezeko la faida kabla ya kodi kwa asilimia 36, kutoka kiasi cha  TZS bilioni 67.8 mwaka uliopita hadi TZS bilioni 92.2 mwaka 2023.

Ikiashiria maendeleo mazuri ya benki hiyo, ripoti hiyo imeonyesha ongezeko la asilimia 6 kwenye Mapato ya Jumla (Total Revenue) ambayo yalipanda kutoka kiasi cha TZS bilioni 236.7 mwaka 2022 hadi TZS bilioni 251.2 mwaka 2023.

 

Akizungumzia taarifa hiyo mwishoni mwa wiki, Afisa Mkuu wa Fedha (CFO) wa benki ya Exim Bw Shani Kinswaga alisema mafanikio hayo yanadhihirisha uimara wa benki hiyo sokoni na zaidi unasisitiza azma yake thabiti katika utoaji wa huduma bora za kibenki.

 

"Ukuaji huu wa faida kipekee unawakilisha azma yetu ya kutoa huduma bora na uwezo wetu wa kuongeza thamani kwa wadau wetu wakiwemo wateja wetu. Mafanikio haya ni matokeo ya mkakati wetu katika kuongeza zaidi vyanzo vya mapato na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa taasisi hii’’ alibainisha Kinswaga.

 

Zaidi, kupitia ripoti hiyo benki ya Exim imeshuhudia ongezeko kubwa la  Amana za Wateja, kutoka  kiasi cha TZS trilioni 1.8 mwaka 2022 hadi TZS trilioni 2.4 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 32. "Ongezeko la Amana hizi linathibitisha sifa ya Exim katika utoaji wa huduma za kibenki zenye  kuaminika na zenye uaminifu kwa wateja wetu tunaowathamini," aliongeza Kinswaga.

 

Hata hivyo jitihada za benki hiyo katika kusaidia sekta mbalimbali za uchumi na kukuza maendeleo endelevu nchini zimezaa matunda, kwani mikopo na kiwango cha utoaji wa mikopo hiyo kiliongezeka kutoka kiasi cha TZS trilioni 1.2 mwaka 2022 hadi TZS trilioni 1.5 mwaka 2023, ikiwakilisha ongezeko lenye kuridhisha la asilimia 22.

 

Kwa upande wa mali, Exim ilishuhudia ukuaji mkubwa katika jumla ya Mali zake, kutoka thamani ya TZS trilioni 2.4 mwaka 2022 hadi TZS trilioni 3.0 mwaka 2023, ikiashiria ukuaji wa asilimia 26. Mafanikio haya yanatajwa kuwa yanaimarisha zaidi msimamo wa kifedha wa benki hiyo na hivyo kuthibitisha uwezo wake imara kwenye uendeshaji wa  shughuli zake.

 

"Kana kwamba hiyo haitoshi, Hisa za Wanahisa wetu ziliongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka kiasi cha  TZS bilioni 264.5 mwaka 2022 hadi TZS bilioni 313.7 mwaka 2023, likiwa ni ongezeko la asilimia 19. Mafanikio haya yanadhihirisha imani na uaminifu ambao wanahisa wetu wanao kutokana na  mwelekeo na usimamizi wetu," aliongeza Kinswaga.

 

Zaidi ya mafanikio yake ya kifedha, katika kipindi cha mwaka 2023, Exim iliendelea kuwekeza zaidi jitihada zake katika eneo zima la Uwajibikaji wa kwa jamii (CSR) ikiongozwa na mpango wake endelevu unaofahamika kama Exim Cares. Uwekezaji wa benki hiyo na uungaji mkono wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ulichangia kuongeza kasi katika maendeleo ya nyanja hizo muhimu nchini ikiwemo sekta ya afya, mazingira sambamba na kuwajengea uwezo wajasariamali hususani wanawake.

 

Kwa upande wa miundombinu, katika kipindi cha mwaka huo benki hiyo iliboresha mfumo wake mkuu wa huduma za kibenki ikilenga kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wake. Mfumo huo mpya ulilenga kurahisisha uchakataji wa miamala, kuongeza usalama, kutoa huduma za kibenki bila vikwazo ili kuwawezesha wateja kufurahia huduma za kifedha kwa urahisi na utulivu.

 

"Hatua hiyo muhimu inathibitisha azma yetu ya kutoa huduma zaidi ya mazoea ya kawaida katika utoaji wa huduma za kibenki," alisema.

 

Kufuatia mafanikio hayo, Kinswaga alielekeza shukrani zake kwa wafanyakazi, wateja na wanahisa wa benki hiyo akisema, "ushirikiano wetu wa pamoja, pamoja na azma yetu ya ubunifu, uzingatiaji wa mahitaji ya wateja, na ufanisi wetu kwenye utoaji wa huduma zetu vimekuwa ndio msingi wa mafanikio yetu. Tutaendelea kuweka kipaumbele zaidi kwenye maeneo haya ili kuchochea ukuaji endelevu na kuunda thamani ya muda mrefu kwa wadau wote." 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...