Na. Damian Kunambi, Njombe.

Kufuatia kuwepo kwa akiba ya eneo lenye ukubwa wa Hekta 297,925 ambayo ni sawa na 66% linalofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali wilayani Ludewa mkoani Njombe Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius sambamba na Mkuu wa wilaya Victoria Mwanziva wametoa wito kwa wawekezaji mbalimbali wa sekta ya kilimo hapa nchini na nchi za jirani kufanya uwekezaji wilayani humo.

Wito huo umetolewa katika mkutano wa wadau wa kilimo mara baada ya kuwasilishwa taarifa ya idara ya kilimo iliyosomwa na afisa kilimo wa wilaya hiyo Godfrey Mlelwa na kueleza kuwa wilaya hiyo ina jumla ya hekta 465,030 zinazofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali lakini mpaka sasa hekta 167,105 sawa na asilimia 34% pekee ndizo zinazolimwa na kupelekea kubakiwa na ziada hiyo ya Hekta 297,925.

"Wilaya imegawanyika katika kanda tatu za uzalishaji ambazo ni ukanda wa juu, ukanda wa kati na ukanda wa chini na mazao ya biashara yanayostawi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ni Kahawa, Parachichi, Chai, Pareto, Korosho na Alizeti", amesema Mlelwa.

Ameongeza kuwa ukanda wa juu huzalisha zaidi Ngano, Mahindi, Maharage, Viazi Mviringo, mboga, Kahawa, Pareto, Chai, Parachichi, Peas na Apple/tofaa ukanda wa kati Mahindi, maharage, Njegere, viazi vitamu, Viazi Mviringo, mboga, Pareto, alizeti, kahawa, Karanga Miti, Karanga, Soya, maembe na Migomba huku ukanda wa chini ukizalisha Mpunga, mhogo, mtama, Ufuta, Viazi vitamu, mboga, korosho, karanga, maembe, ndizi na machungwa.

Aidha mkuu wa wilaya Victoria Mwanziva amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samaia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza uboreshaji wa sekta ya kilimo kwa vitendo ambapo kwa wilaya ya Ludewa ametoa pikipiki 58 kwaajili ya maafisa ugani ili waweze kuwafikia wakulima kwa urahisi sambamba kutoa vifaa vya kupima udongo ambavyo maafisa ugani hao huvitumia kuwapimia udongo wakulima katika maeneo yao pasipo malipo yoyote.

" Ndugu zangu tuna kila sababu ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwajibika kila mtu kwa nafasi yake kwani sisi kama wilaya na halmashauri tumehakikisha wakulima wetu wanapata pembejeo kwa wakati na kuwaimarishia masoko tumeendelea kuimarisha vyama vya ushirika kwani kwa kufanya hivyo mkulima ataendelea kuinuka na kukuza uchumi wake binafsi,wilaya na nchi kwa ujumla", amesema Mwanziva.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius amesema pamoja na kuhitaji wawekezaji katika kilimo lakini pia wanahitaji mazao yanayozalishwa wilayani humo yaweze kuongezewa thamani ambapo badala ya kusafirisha mazao ghafi yasafirishwe yaliyosagwa kabisa kama zao la mahindi, chai, kahawa, pareto,halizeti na mazao mengineyo hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kupata wawekezaji wa mashine mbalimbali.

Gervas Ndaki ni katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilayani humo amesema kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020/2025 ibara ya 37 imeeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano chama hicho kitasimamia mapinduzi katika sekta ya kilimo na kuhakikisha kinakuwa kilimo chenye tija na kinachotumia teknolojia ya kisasa.

"Kila tunachokifanya ni utekelezaji wa ilani yetu ya uchaguzi kwani imetuambia tutambue maeneo na aina ya kilimo kinachokubali katika maeneo husika na imeweka msisitizo huu kwakuwa asilimia 65 ya watanzania wote ni wakulima hivyo kilimo ni chanzo kikubwa cha uchumi wetu hivyo hatuna budi kukitilia mkazo katika kuboresha kilimo hiki", amesema Ndaki.

Wanachama wa vyama vya ushirika ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huo wamepongeza hatua hiyo iliyofikiwa na serikali huku wakiomba mikutano hiyo kufanyika mara kwa mara ili kuweza kupata maarifa zaidi juu ya kilimo cha mazao mbalimbali wilayani humo.

Christopher Mgimba ni miongoni mwa wanachama hao wa ushirika ameipongeza serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kutokomeza wadudu aina ya viwavi jeshi mashambani mwao mara tu walipo bainika tena pasipo malipo yoyote kwani imesaidia mazao yao kukua kwa ubora kwani endepo hatua hizo zisinge chukuliwa mazao mengi yangeharibiwa na wadudu hao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...