Na Benny Mwaipaja, DSM
Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameishukuru
Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia (Millennium
Challenge Corporation-MCC) kwa kuiteua Tanzania kuwa moja ya nchi
zilizoko kwenye mpango wa kunufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia
mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi.
Dkt.
Nchemba amesema hayo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya
mazungumzo na ujumbe wa Shirika hilo la Changamoto za Milenia-MCC,
ukiongozwa na Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wake, Bi. Chidi Blyeden.
Aliueleza
ujumbe huo kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kusimamia uchumi
wake, masuala ya utawala bora, haki za binadamu, demokrasia, na kwamba
imetekeleza kwa kiwango kikubwa vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo ili
nchi iweze kunufaika na mpango huo.
Dkt.
Nchemba aliishukuru MCC kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya
nchi ambapo kupitia Mradi wa Changamoto za Milenia uliotekelezwa nchini
kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2008 hadi 2013, uliiwezesha Tanzania
kupata dola za Marekani 698 milioni, zilizotumika kutekeleza miradi
katika sekta za usafirishaji, nishati na maji.
“Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameituliza nchi kisiasa, na kuwa na nia
ya dhati ya kuituliza nchi kwa kuruhusu masuala ya kisiasa kufanyika kwa
uwazi na hata hii si tu kwa ajili ya kutekeleza vigezo vya taasisi
yoyote bali ni nia yake ya dhati ya kulinda uhuru wa watu” alisema Dkt.
Nchemba.
Kwa
upande wake, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Changamoto za
Milenia (MCC), Bi. Chidi Blyeden, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa
ilizopiga katika kuimarisha masuala ya utawala bora, demokrasia na haki
za binadamu chini ya utawala wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua
iliyolifanya Shirika lake kurejesha ushirikiano na Serikali.
Bi.
Blyeden alieleza kuwa Wataalam kutoka MCC wanaendelea na mijadala na
wataalam wa Serikali ili kuharakisha kuanza kwa utekelezaji wa mpango
huo ambao matokeo yake hapo baadae utaiwezesha Marekani kurejesha mradi
wa Changamoto za Milenia (MCC-Compact) ambao utakuwa na lengo la
kusaidia nchi kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.
Mwezi
Desemba mwaka 2023, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC),
ilizichagua Tanzania na Philippines, kama wabia wake katika kuandaa
programu za awali (threshold programs) zitakazolenga katika mageuzi ya
kisera na kitaasisi ambazo nchi hizi zinaweza kuyafanya ili kupunguza
umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Bodi
hiyo ya MCC ilichukua uamuzi huo baada ya Tanzania na Ufilipino,
kuonesha dhamira mpya ya kusukuma mbele mageuzi muhimu ya kuimarisha
utawala wa kidemokrasia, kulinda haki za binadamu na kupambana na
rushwa.
Shirika
la Changamoto za Milenia (MCC), ni shirika huru la Serikali ya Marekani
linalojielekeza kupunguza umaskini duniani kupitia ukuaji wa kiuchumi,
kwa kutoa ruzuku na misaada ya muda maalum kwa nchi zinazokidhi viwango
na vigezo thabiti vya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na
kuheshimu haki za kidemokrasia.
Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akisalimiana na
Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Changamoto za Milenia
(Millennium Challenge Corporation-MCC), Bi. Chidi Blyeden, walipokutana
na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika hilo kuhusu namna Tanzania
itakavyotekeleza na kunufaika na mpango wa ruzuku zinazolenga kusaidia
mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji uchumi
(Threshold Programs), mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Hazina
Ndogo, Jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Balozi wa
Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza na Mwakilishi wa Tanzania wa
Mradi wa MCC Dkt. Hamisi Mwinyimvua.Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-dar es Salaam
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...